Cuba yajitayarisha kwa kipindi cha maombolezi
27 Novemba 2016Majivu ya Castro watazikwa katika mji wa Santiago de Cuba baada ya siku nane za maombolezi rasmi ya kitaifa, ambayo yanatarajiwa kufikia mwisho Desemba 4.
Umma utaruhusiwa kushuhudia mwili wa Castro Jumatatu na Jumanne , katika eneo la makumbusho la Jose Marti mjini Havana , na kisha kutakuwa na sala maalum ya kumuaga siku ya Jumanne katika uwanja mkuu wa mapinduzi mjini humo.
Gwaride nchi nzima litafuatia katika muda wa siku nne, kwa matembezi ya jumla ya kilometa 900 kutoka mji mkuu wa Cuba Santiago, na mkutano mkubwa wa pili wa sala utafanyika siku ya Jumamosi.
Maafisa wa Cuba wamesema tukio la mazishi linatarajiwa kufanyika katika makaburi ya Santa Ifigenia mjini Santiago Desemba 4.
Mshairi na mwanasiasa wa jamhuri Jose Marti pia amezikwa hapo. Katika kipindi cha maombolezi hakutakuwa na shughuli ama matamasha ya wazi , bendera zitapepea nusu mlingoti katika majengo ya serikali na radio na televisheni zitatangaza vipindi vya taarifa, uzalendo na historia, maafisa wamesema.
Picha za hivi karibuni zilizochapishwa za Fidel Castro zilikuwa za Novemba 15, wakati alipokutana na rais wa Vietnam Tran Dai Quang. Tukio lake la mwisho kuonekana hadharani lilikuwa Agosti 13 katika ukumbi wa matamasha wa Karl Max mjini Havana. Tangu kuondoka madarakani mwaka 2006, Fidel Castro alijing'atua kutoka katika siasa halisi.
Kifo cha Castro usiku wa Ijumaa akiwa na umri wa miaka 90 kilitangazwa katika televisheni ya taifa na mdogo wake wa kiume Raul Castro. Afya ya Castro iliwekwa siri kwa kiasi kikubwa nchini Cuba. Hakuna taarifa iliyotolewa kuhusiana na sababu za kifo chake.
Mahasimu wafurahia kifo cha Castro
Wakati huo huo Wamarekani Wacuba walimiminika mitaani mjini Miami siku ya Jumamosi (26.11.2016) wakiimba "Cuba Libre!" na "Uhuru ! Uhuru !" wakati wakisherehekea kifo cha adui yao mkubwa Fidel Castro.
Watu hao waliokuwa wakisherehekea , wengi wao waliukimbia utawala wa kikomunist wa Havana walipiga honi, kupiga sufuria na ngoma , na kucheza, wakilia , na kupeperusha bendera ya Cuba katika hali ya furaha kubwa katika jamii hiyo.
Mjini Miami , ambako wanaishi Wamarekani Wacuba wengi nchini Marekani, taarifa hizo zilisambaa haraka kwa hamasa. "Ni masikitiko kwamba mtu anafurahia kifo cha mtu mwingine , lakini mtu huyu hakupaswa kuzaliwa," alisema Pablo Arencibia , mwenye umri wa miaka 67, mwalimu ambaye alikimbia kutoka Cuba miaka 20 iliyopita.
Wakitanabahi kuhusu tukio la kihistoria , vijana waliokuwa wakifurahia waliweka tukio hilo moja kwa moja katika ukurasa wa Facebook, waliweka picha katika ukurasa wa Instagram, na walionesha sherehe hizo katika Face Time na Skype kwa marafiki na ndugu katika kisiwa hicho.
Havana ndogo na Hialeah , maeneo ambako Wacuba wengi wanaoishi uhamishoni wanaishi , waliona watu wakicheza, kukumbatiana , na kuzungumza, kwa kusema "ilichukua muda mrefu sana ," na "sasa ni zamu ya Raul."
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / dpae
Mhariri: Mwehozi, Sylvia