1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Cyprus na rais Joachim Gauck magazetini

25 Machi 2013

Mgogoro wa Cyprus, na ziara ya rais wa shirikisho la jamhuri ya Ujerumani Joachim Gauck nchini Italia ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani .

Rais Gauck (kushoto) na rais Giorgio Napolitano wa Italia wakizuru makaburi ya wahanga wa vita vikuu vya pili katika mkoa wa Lucca huko TuscanaPicha: picture alliance / dpa

Tuanzie lakini na kishindo kinachoikaba Cyprus. Hatimae viongozi wa serikali ya mjini Nicosia wameridhia masharti ya wafadhili na kuepukana na balaa la kufilisika. Hata hivyo wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanahofia hali kama hiyo iliyoisibu Cyprus inaweza kuifika nchi yoyote ile nyengine ya kanda ya Euro. Gazeti la "Straubinger Tagblatt/Landshuter Zeitung linaandika:Hata kama mjini Brussels viongozi hawachoki kusisitiza kwamba kuwawajibisha wateja wa benki si hatua itakayopitishwa kila wakati, hata hivyo wasiwasi mkubwa umeenea. Pengine mnamo siku au wiki zijazo Wataliana na Wahispania pia watajikuta wakitoa akiba zao kutoka benki. Kwa sababu hata katika nchi hizo mgogoro unasababishwa kwa sehemu kubwa na benki. Zikilinganishwa na Cyprus, tofauti si kubwa hivyo.

Gazeti la "Rhein-Necker-Zeitung" linaandika:Nini kinawasumbua Wajerumani, Wahispania au Wafaransa ikiwa matajiri wa Urusi watalazimika kutoa moja kwa tano ya fedha zao walizoweka katika benki za Cyprus? Kila mmoja angesema: Hakuna. Kimsingi lakini jibu lingebidi liwe "Kipo", kwa sababu kichinichini mtindo huo wa kuwalazimisha wateja wawajibike unawafanya watu wapoteze imani. Hata nchini Ujerumani kuna kifungu kinachosema akiba ya hadi Euro laki moja ni salama. Wiki kama moja hivi iliyopita, na kwa sababu ya mgogoro wa Cyprus, Kansela Angela Merkel na waziri wake wa fedha Wolfgang Schäuble walikuwa tayari kuivunja ahadi hiyo inayotumika katika nchi zote za kanda ya Euro.

Kitisho cha DM chaibuka upya

Noti ya sarafu ya zamani ya Ujerumani:DM 100Picha: Fotolia/Eva Kahlmann

Gazeti la "Stuttgarter Zeitung" linahisi hofu walizokuwa nazo baadhi ya watu kutokana na nguvu za sarafu ya zamani ya Ujerumani, "Deutsche Mark" hazaijatoweka licha ya sarafu ya pamoja ya Euro. Gazeti linaendelea kuandika:Kiroja kikubwa cha kihistoria kinashuhudiwa: Euro, ambayo ndiyo iliyokuwa ibuni aina mpya ya mshikamano barani Ulaya, ndio inayosababisha watu kugongana vichwa. Na hasa katika zile nchi ambako watu walitarajia kumalizika enzi za Deutsche Mark ingekuwa chanzo cha kutoweka maguvu ya kiuchumi ya Ujerumani, ndiko huko huko ambako sauti zinapazwa dhidi ya nguvu za kiuchumi za Ujerumani. Kufumba na kufumbua "usemi wa tangu zamani umerejea tena midomoni: Eti Wajerumani wanajisikiaje ?

Gazeti la "Neue Osnabrücker Zeitung" linazungumzia kuhusu ziara ya rais wa shirikisho la jamhuri ya Ujerumani Joachim Gauck nchini Italia ambako aliyazuru makaburi ya wahanga wa mauwaji ya utawala wa zamani wa Wanazi. Gazeti linaendelea kuandika:Ni wajibu na jambo la lazima kwa rais wa shirikisho la jamhuri ya Ujerumani Joacjim Gauck kuwapigia magoti wahanga 560 - raia wa Italia waliouliwa na wanajeshi wa utawala wa Wanazi mnamo mwaka 1944 katika kijiji kimoja cha Toscana. Mauwaji hayo yanatoa mfano wa shida zinazowapata watu katika kukabiliana na uhalifu uliotokea.Italia, kutokana na sababu za kisiasa katika enzi za Vita Baridi, haikutoa maelezo mengi. Kuanzia mwaka 1994 ndipo nyaraka zilipoweza kugunduliwa katika maktaba ya ofisi ya mwendesha mashtaka mkuu wa kijeshi. Baadae ndipo wachunguzi walipoanza shughuli zao na matokeo waliyoyapata hayakuridhisha. Yote hayo Gauck alikuwa akiyajua. Hata hivyo anasema "Makosa ni makosa hata kama hayakudhihirika kisheria.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Mohammed Khelef

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi