Cyprus yahaha kuepuka kufilisika
24 Machi 2013Yakikabiliwa na muda wa mwisho siku ya Jumatatu kuzuia kuanguka kwa mfumo wa benki wa Cyprus, mazungumzo yanayolenga kufikia muafaka juu ya mpango wa uokozi kutoka Umoja wa Ulaya na shirikka la fedha la kimataifa IMF mjini Nicosia yalivunjika usiku wa Jumamosi bila matokeo. Taarifa ya serikali ya Cyprus ilisema mazungumzo yapo katika hatua ngumu sana, na kuongeza kuwa hali ni ngumu sana na muda umebaki mchache sana. Anastaciades alitarajiwa mjini Brussels asubuhi ya leo (24.03.2013)kuendelea na mazungumzo, ilisema taarifa hiyo.
Maelezo ya taarifa ilitofautiana sana na matumaini ya tahadhari wakati wa siku za majadiliano makali kati ya viongozi wa Cyprus na maafisa kutoka pande tatu za wakopeshaji - Umoja wa Ulaya, IMF na Benki Kuu ya Umoja wa Ulaya. Huku sekta ya benki ya nchi hiyo, ambayo ni kubwa kuliko nchi yenyewe ikiwa imeporomoka kutokana na kuhusishwa na mfumo wa nchi iliyokumbwa na misukosuko ya Ugiriki, Umoja wa Ulaya unasema kisiwa hicho kilichopo mashariki mwa bahari ya Mediterannean laazima kitafute euro bilioni 5.8 kivyake, kabla ya kupatiwa fedha za uokozi kiasi cha euro bilioni 10.
Bila kuwepo na makubaliano siku ya Jumatatu, Benki ya Umoja wa Ulaya ECB, inasema itasitisha utoaji wa fedha za dharura kwa benki za Cyprus, hatua inayoweza kuuangusha mfumo wa benki nchini humo na hatimaye kuondolewa katika kanda inayotumia sarafu ya euro. Kiongozi wa kihafidhina Anastaciades, ambaye hana hata mwezi moja madarakani, na anaekabiliwa na mgogoro mbaya zaidi nchini Cyprus tangu uvamizi wa vikosi vya Uturuki mwaka 1974 uliyokigawanya kisiwa hicho mara mbili, anatarajiwa kukutana na viongozi wa Umoja wa Ulaya, Benki Kuu ya Umoja wa Ulaya na IMF. Mawaziri wa fedha wa mataifa 17 yanayotumia sarafu ya euro watakutana jumapili jioni.
Wakihangaika kutafuta fedha, maafisa wa Cyprus walikubaliana juu ya kodi ya mara moja kwa fedha zaidi ya euro laki moja zinazowekwa benki, msimamo ambao ni tofauti na siku tano nyuma, wakati wabunge walipotupilia mbali pendekezo kama hilo waliloliita wizi wa benki. Afisa mwandamizi wa Cyprus alisema serikali mjini Nicosia ilikubaliana na wakopeshaji juu ya kodi ya asilimia 20 kwenye fedha zinazofikia euro laki moja na zaidi kwa mkopeshaji mkubwa zaidi nchini humo, Benki ya Cyprus, na asilimia nne kwenye fedha za kiwango sawa katika mabenki mengine.
Ni chaguo ngumu tu zilizosalia
Waziri wa fedha Michael Sarris alizungumzia juu ya maendeleo muhimu katika mazungumzo ya asubuhi, wakati ambapo waandamanaji wenye hasira waliokuwa nje ya wizara yake wakiimba nyimbo za kumtaka ajiuzulu. Kamishna wa masuala ya uchumi wa Umoja wa Ulaya Olli Rehn alisema kulikuwepo na maendeleo, lakini alionya juu ya wakati mgumu huko mbele. "Kwa bahati mbaya matukio ya siku za hivi karibuni yamepelekea hali ambapo hakuna tena suluhu zenye unafuu," alisema katika taarifa na kuongeza kuwa, "leo hii tumebakiza tu chaguo ngumu."
Katika kura ya kushangaza siku ya Jumanne, bunge la Cyprus lenye wabunge 56 lilikataa kutozwa kodi kwa wateja wa benki, wakubwa na wadogo, na Sarris alitumia siku tatu zisizo na mafanikio mjini Moscow akijaribu kutafuta msaada kutoka Urusi, ambayo raia wake wana mabilioni ya euro yaliyo hatarini katika benki za Cyprus. Baada ya kutolewa nje na utawala wa Kremlin, Sarris alisema kodi hiyo imerudishwa kwenye meza.
Siku ya Ijumaa wabunge walipiga kura usiku wa manane kutaifisha mifuko ya hifadhi ya jamii na kugawanya wakopeshaji kati ya mabenki mazuri na mabaya - hatua ambayo inaweza kutumika kwa benki ya pili kwa ukopeshaji ya Cyprus Popular Bank, ambayo inajulikana pia kama Laiki. Ripoti za vyombo vya habari vya Cyprus zilisema kuwa mazungumzo yalikwama juu ya matakwa ya IMF kuwa Benki ya Cyprus ichukuwe mali nzuri za mshindani wake Popular Bank na kuhamisha deni lake la euro bilioni tisa kwa benki kuu pia. Ripoti hizo zilisema serikali bado ilikuwa inapinga matakwa hayo.
Tayari mpango wa Cyprus wa kuchukua fedha kutoka mifuko ya hifadhi ya jamii uliwekwa pembeni kufuatia upinzani kutoka Ujerumani, ambayo ilionya kuwa hatua hiyo inaweza kusababisha maumivu zaidi kwa raia wa kawaida kuliko kutozwa kodi kwa fedha zinazowekwa benki. Ilikuwa pia haitabiriki iwapo wabunge wengi wataunga mkono kodi iliyofanyiwa marekebisho, au kama serikali inaweza kujaribu kulizunguka bunge.
Wacyprus wa kawaida wamekasirishwa na kodi hiyo na kushangazwa na kasi ya kutokea kwa mambo. Walimchagua Anastaciades mwezi Februari kwa ahadi ya kupata uokozi na kunusuru benki ambazo mtaji wake ulifutwa na uwekezaji nchini Ugiriki, ambayo ndiyo nchi ulikoanzia mgogoro wa madeni wa kanda inayotumia sarafu ya euro.
Hofu ya uchukuaji mkubwa wa fedha
Lakini katika wiki iliyopita raia hao wamekuwa wakivamia mashine ya kutolea fedha tangu mabenki yalipofunga milango kwa amri ya serikali, ili kuzuia uhamishaji mkubwa wa fedha nje ya nchi. Kwa kutarajia wateja wengi kuchukua fedha kwa wingi kutoka mabenki kwa wakati mmoja yatakapofunguliwa siku ya Jumanne, bunge lilitoa mamlaka kwa serikali kuweka hatua za kudhibiti utoaji wa fedha. Siku ya Jumamosi karibu waandamanji 1,500 wengi wao wakiwa wafanyakazi wa benki walielekea ofisi ya rais wakiwa na mabango yanayosomeka "hapana kwa ufilisi wa Cyprus" na "hakuna kugusa mifuko ya ustawi wa wafanyakazi."
Kodi kwa fedha zinazowekwa benki inawakilisha hatua isiyo kifani katika ushughulikiaji wa mgogoro wa madeni barani Ulaya, ambao umesambaa kutoka Ugiriki hadi Ireland, Ureno, Uhispania na Italia. Viongozi wa Cyprus hapo awali walijaribu kusambaza maumivu kati ya wateja wakubwa na wadogo, kwa kuhofia madhara ambayo wangeisababishia nchi kama sehemu salama ya kuwekwa fedha kwa matajiri wa kigeni, wengi wao wakiwa Warusi na Waingereza.
Mabenki hayo yanayotitia sasa yana kiasi cha euro bilioni 68, zikihusisha euro bilioni 38 zilizopo katika akaunti zilizo na zaidi ya euro 100,000 - viwango ambavyo ni vikubwa kwa kisiwa hicho chenye wakaazi milioni 1.1, ambacho kisingeweza kumudu mfumo huo mkubwa wa fedha kivyake. "Mabenki ya Cyprus kwa miaka mingi yamekuwa yakichukua hatari ambazo haziruhusiwi nchini Ufaransa," gavana wa Benki Kuu ya Ufaransa Christian Noyer aliliambia gazeti la Ufaransa la Le Journal Du Dimanche. "Hakuna mtu anataka Cyprus iache kanda ya euro," alisema na kuongeza kuwa watu wa kwanza kuteseka watakuwa raia wa Cyprus.
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/rtre
Mhariri: Sekione Kitojo