1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ramaphosa aahidi kupambana na rushwa

Isaac Gamba
17 Februari 2018

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa  ametoa hotuba yake ya kwanza kwa taifa hapo jana Ijumaa ikiwa ni siku moja baada ya kuapishwa kuwa rais  mpya wa taifa hilo kufuatia kujiuzulu kwa Jacob Zuma.

Südafrika - neuer Präsident Cyril Ramaphosa
Picha: Getty Images/AFP/M. Hutchings

 

Akilihutubia taifa kupitia bunge la nchi hiyo  na huku akipigiwa makofi na kushangiliwa  Ramaphosa alitoa mwito kwa wananchi wa Afrika Kusini kuweka kando tofauti zote miongoni mwao ambazo zimeliathiri taifa hilo na kuanza sasa mwanzo mpya.

Mwanzoni mwa hotuba yake Ramaphosa alimsifia mtangulizi wake Jacob Zuma kwa utendaji wake kwa taifa na kuibua sauti za miguno kutoka kwa baadhi ya wabunge. Hata hivyo Zuma hakuwepo bungeni wakati wa hotuba hiyo hapo jana.

Ramaphosa ambaye alikuwa makamu wa rais chini ya utawala wa rais Jacob Zuma  amesema utawala wake utajikita zaidi katika kutengeneza ajira pamoja na kuvutia uwekezaji  na kwamba ni muda muafaka sasa kwa taasisi za umma pamoja na viongozi kurejesha imani iliyokuwa inaanza kutoweka.

Amesema  mwaka huu serikali yake itapambana na vitendo vya rushwa katika taasisi za umma na kuongeza kuwa  idara zinazohusika na kuzuia vitendo vya uhalifu zimekuwa zikichukua hatua  ambazo zitasaidia kupambana ipasavyo na rushwa.

Ramaphosa  ambaye wakati wa hotuba hiyo  alionekana kuwa mtulivu na  mwenye bashasha  alisema tume maalumu kwa ajili ya kufanya uchunguzi katika taasisi mbalimbali inatarajia kuanza kazi yake hivi karibuni  na kuwa wote wanaohusika na vitendo vya kifisadi watafichuliwa.

Wanachi Afrika Kusini waonesha matumaini kwa Ramaphosa

Walio wengi nchini Afrika Kusini wanamatumaini kuwa Ramaphosa mmoja wa wanaharakati wa ukombozi wa taifa hilo kutoka kwa utawala wa wazungu wachache ataleta mageuzi nchini humo baada ya kukithiri kwa kashfa za rushwa, ambazo zimepunguza umaarufu wa chama tawala cha African National Congress (ANC).

Miongoni mwa tuhuma zilizokuwa zikimuandama mtangulizi wa Ramaphosa, Jacob Zuma, ni pamoja na kuruhusu familia ya wafanyabiashara maarufu nchini humo ya Gupta kujipatia  mikataba mikubwa ya kibiashara na pengine hata familia hiyo kushawishi uteuzi wa nafasi kadhaa katika baraza la mawaziri nchini humo.

Julius Malema kiongozi wa chama cha upinzani cha Economic Freedom Fighters alisema baada ya hotuba hiyo kuwa anakaribisha baadhi ya ahadi za Ramaphosa zinazohusiana na kupambana na rushwa na kuongeza kuwa walikuwa na tatizo na kiongozi aliyepita akimaanisha Zuma na kuwa sasa tatizo limeondoka.

Zuma ambaye anaweza akakabiliwa na mashtaka alionekana kutojali hadi wakati alipojiuzulu Jumatano wiki hii huku akisema hatambui kosa alilofanya. 

Katika siku chache tangu Jacob Zuma kujiuzulu polisi wamewakamata watu kadhaa wanaodaiwa  kuhusika na ufisadi katika mashirika ya umma na mmoja wa watendaji wakuu katika shirika linalotoa huduma ya umeme linalomilikiwa na serikali, ambaye pia alikuwa akichunguzwa,  amejiuzulu.

Mwandishi: Isaac Gamba-dpae/ape

Mhariri: Yusra Buwayhid

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW