1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UhalifuAfrika

Daktari ashtakiwaUfaransa kwa mauaji ya kimbari ya Rwanda

14 Novemba 2023

Daktari mmoja raia wa Rwanda amefikishwa mahakamani nchini Ufaransa Jumanne kwa tuhuma za mauaji ya kimbari na uhalifu dhidi ya binadamu wakati wa mauaji ya mwaka 1994 nchini mwake, baada ya uchunguzi wa muda mrefu.

Mafuvu na picha za baadhi ya wahanga wa mauaji ya Kimbari ya Mwaka 1994.
Mafuvu na picha za baadhi ya wahanga wa mauaji ya Kimbari ya Mwaka 1994.Picha: Ben Curtis/AP/picture alliance

Sosthene Munyemana mwenye umri wa miaka 68 alifikishwa mbele ya Mahakama ya Assize katika mji mkuu wa Ufaransa karibu miaka 30 baada ya malalamiko kuwasilishwa dhidi yake katika mji wa kusini magharibi mwa Ufaransa wa Bordeaux mwaka 1995.

Daktari huyo wa zamani wa magonjwa ya wanawake, anayetuhumiwa kuandaa mateso na mauaji wakati wa mauaji ya kimbari ya Watutsi nchini Rwanda, alifika kwa kuchelewa katika kesi hiyo.

Soma pia: Mtuhumiwa mauaji ya kimbari Rwanda kufikishwa Mahakamani Ufaransa

Akiwa amevalia shati la mistari ya bluu na koti la kijivu, Munyemana aliomba msamaha kwa kuchelewa, kabla ya kutaja utambulisho wake. Ameishi Ufaransa tangu 1994. Munyemana, ambaye anakanusha mashtaka hayo, anakabiliwa na kifungo cha maisha jela iwapo atapatikana na hatia.

Kesi hiyo, iliyopangwa kudumu kwa wiki tano, itarekodiwa kwa ajili ya kumbukumbu za kihistoria. Karibu mashahidi 70 wanatarajiwa kutoa ushahidi.

Nguo za baadhi ya waliochinjwa wakati wa mauaji ya kimbari wakati wakitafuta hifadhi ndani ya Kanisa, zikinin'ginia juu ya majeneza ya mabaki ya wahanga kama kumbukumbuku kwa waliouawa katika eneo la Ntarama, Rwanda.Picha: Ben Curtis/AP/picture alliance

Ni kesi ya sita nchini Ufaransa kwa wanaodaiwa kuhusika katika mauaji hayo, ambapo takriban watu 800,000, wengi wao wakiwa wa kabila la Watutsi, walichinjwa kwa muda wa siku 100.

"Tunasubiri haki itendeke mwishowe," Rachel Lindon, wakili anayewakilisha wahanga 26, alisema kabla ya kesi hiyo kuanza. "Kadiri muda unavyopita, ndivyo tunavyokuwa na mashahidi wachache," aliongeza.

Sababu za kucheleweshwa kwa uchunguzi

Marc Sommerer, rais wa Mahakama ya Assize, alitaja sababu za kuredushwa kwa uchunguzi huo kwa mambo kadhaa ikiwa ni pamoja na "haja ya kufanya uchunguzi nje ya nchi" na kwamba Ufaransa ilianzisha kitengo cha uhalifu dhidi ya ubinadamu tu mwaka 2012.

Soma pia: Rwanda yakosolewa kwa vitisho na mauaji ya wakosiaji ugenini

Lakini pia mwaka 2010 ilikataa ombi la kurejeshwa kutoka kwa Rwanda baada ya mawakili wa Munyemana kudai kuwa hawezi kupata kesi ya haki huko.  Mnamo 2011, mahakama ya Ufaransa ilimshtaki baba huyo wa watoto watatu kwa tuhuma kwamba alishiriki katika mauaji ya kimbari ya 1994.

Munyemana, kutoka kabila Wahutu, aliishi Butare kusini mwa Rwanda wakati huo.  Alikuwa karibu na Jean Kambanda, mkuu wa serikali ya mpito iliyoanzishwa baada ya kudunguliwa kwa ndege iliyokuwa imembeba kwa kombora mwaka 1994.

Ufaransa imekuwa mojawapo ya maeneo yanayoongoza kwa wakimbizi wanaokimbia haki kutokana na mauaji ya Rwanda. Rwanda chini ya Rais Paul Kagame imeishutumu Paris kwa kutokuwa tayari kuwasafirisha washukiwa wa mauaji ya kimbari au kuwafikisha mahakamani.

Rais wa Rwanda Paul Kagame akiwasha mwanga wa kumbukumbu ya 29 mauaji ya kimbari ya 1994, Aprili 7, 2023.Picha: Mariam Kone/AFP/Getty Images

Tangu 2014, Ufaransa imejaribu na kuwahukumu watu sita ikiwa ni pamoja na mkuu wa zamani wa kijasusi, mameya wawili wa zamani na dereva wa zamani wa hoteli.

"Alikuwa daktari, mtu mashuhuri ambaye alithaminiwa sana," Emmanuel Daoud, mwanasheria wa Shirikisho la Kimataifa la Haki za Kibinadamu (FIDH) na Ligi ya Haki za Kibinadamu (LDH), alisema kuhusu Munyemana. "Haiwezekani kuwa alikuwa hajui kinachoendelea," aliongeza.

Soma pia: Makumbusho ya maafa Rwanda yaongezwa katika Turathi za Dunia

Munyemana anatuhumiwa kusaidia kuandaa barua ya kuunga mkono serikali ya mpito, ambayo ilihimiza mauaji ya Watutsi. Pia anatuhumiwa kusaidia kuweka vizuizi vya kuwakusanya watu na kuwaweka katika mazingira yasiyo ya kibinadamu katika ofisi za serikali za mitaa kabla ya kuuawa.

Munyemana anahoji kuwa ofisi za serikali alizoshikilia ufunguo zilitumika kama "kimbilio" la Watutsi waliokuwa wakitafuta ulinzi. Mmoja wa mawakili wa Munyemana, Jean-Yves Dupeux, amedai kuwa kesi hiyo "inategemea tu" maelezo ya mashahidi ya miongo kadhaa.   

Akizungumza na wanahabari siku ya Jumanne, alisema kuwa Munyemana hakushiriki katika mauaji hayo lakini yeye mwenyewe alikuwa hatarini kwa sababu "alikuwa Mhutu mwenye msimamo wa wastani."

Kituo cha kumbukumbu ya mauaji ya kimbari cha mjini Kigali.Picha: Hatim Kaghat/Belga Mag/AFP/Getty Images

Munyemana alifanya kazi kama daktari wa dharura kusini-magharibi mwa Ufaransa kabla ya kugeukia matibabu ya watoto.

Zaidi ya watu 800,000, hasa Watutsi walio wachache, waliuawa kinyama na wanajeshi wa Kihutu na wanamgambo wenye itikadi kali katika mauaji ya kimbari ya Rwanda kuanzia Aprili hadi Julai 1994, kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa.

Chanzo: AFPE

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW