Daktari aliyetoa tahadhari ya mwanzo kuhusu corona afariki
7 Februari 2020Tedros Adhanom Ghebreyesus ambaye ni mkuu wa shirika la afya duniani WHO amesema leo akiwa mjini Geneva kuwa ulimwengu unakumbwa na uhaba mkubwa wa vifaa hivyo vya kuvaa usoni kujikinga dhidi ya maambukizi ya corona.
Tedros amesema mapema wiki hii, shirika lake lilianza kupeleka vifaa hivyo vikiwa ni pamoja na glovu za mikononi, gauni maalum za kujikinga na vifaa vya kupima virusi hivyo katika mataifa yanayohitaji msaada.
Tedros ameongeza pia kuwa baadhi ya nchi zinakosa kutoa taarifa au data kuhusu maambukizi ya virusi hivyo yaliyothibitishwa.
Nchi zinabana taarifa kuhusu maambukizi?
"Ulimwengu unakumbwa na upungufu mkubwa wa vifaa vya kujikinga dhidi ya virusi vya corona. Usiku wa leo nitazungumza na wanaotengeneza vifaa hivyo ili wabaini vizingiti vilivyopo na tupate suluhisho ili kuwe na usawa katika kugawa vifaa hivyo." Amesema Tedros.
Tedros ameeleza pia kuwa katika siku mbili zilizopita, idadi ya maambukizi yaliyoripotiwa imepungua. Amesema hiyo ni ishara nzuri lakini ameonya kutozembea kwani idadi inaweza kuongezeka tena.
Idadi ya watu waliokufa kutokana na virusi hivyo nchini China imepindukia watu 630.
Daktari aliyetoa tahadhari ya mwanzo kuhusu coroa afariki
Miongoni mwa waliokufa ni daktari aliyetoa tahadhari ya mwanzo kuhusu virusi hivyo nchini China Li Wenliang.
Daktari huyo mwenye umri wa miaka 34 na aliyekuwa akifanya kazi katika hospitali ya Wuhan ambao ndio kitovu cha virusi hivyo vipya, alijikuta matatani na serikali ya kikomunisti ya China, baada ya kutoa taarifa hiyo mnamo mwisho wa mwezi Disemba.
Punde baada ya kutoa taarifa kuhusu virusi hivyo, maafisa wa polisi wa China walimkata dakatari huyo kwa madai ya kueneza uvumi kuhusu virusi vya corona.
Pia aliambiwa asaini waraka kama ahadi kuwa atakoma kueneza habari kuhusu virusi vya corona. Daktari Li aliandika kwenye ukurasa wake wa mitandao ya kijamii kuwa alithibitika kuwa na virusi hivyo Februari mosi.
Kifo cha Daktari Li chazusha ghadhabu
Kifo chake kimezusha ghadhabu miongoni mwa watumiaji wa mitandao ya kijamii wanaoishutumu serikali ya China kwa kukosa kuwajibika na pia kwa kumhangaisha Li pamoja na wengine waliotoa taarifa kuhusu virusi hivyo.
Mhariri wa jarida la Global Times la China ambalo huungwa mkono na serikali Hu Xijin, ameandika kwenye mitandao ya kijamii kuwa maafisa wa Wuhan na Hubei wanapaswa kumuomba radhi daktari Li pamoja na watu wa Hubei na taifa zima.
Shirika la Afya Duniani, WHO, limeelezea kusikitishwa sana na kifo cha daktari Li. Kwenye ukurasa wake wa Twitter shirika hilo limeongeza kwamba ulimwengu unapaswa kuipongeza kazi iliyofanywa na daktari huyo katika kudhibiti corona.
Miongoni mwa zaidi ya watu 31,000 walioambukizwa ulimwenguni, zaidi ya watu 28,000 wameambukizwa nchini China pekee. Virusi hivyo vimesambaa katika zaidi ya mataifa 20.
Vyanzo: AFPE