Daktari wa Kongo apokea tuzo ya Sacharow
22 Oktoba 2014Denis Mukwege ni daktari mkuu wa hospital ya Panzi mjini Bukavu, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Kila siku, daktari huyo bingwa anawahudumia wanawake waliodhalilishwa kingono. Daktari Mukwege ni mmoja wa wanaharakati wanaopinga unyanyasaji wa kijinsia unaotumika kama nyenzo ya kivita.
Kwa sababu ya juhudi zake hizo, bunge la Umoja wa Ulaya limemtunukia tuzo ya Sacharow inayotolewa kwa wale wanaotetea haki za binadamu. Spika wa bunge, Martin Schulz, Jumanne alimkabidhi daktari Mukwege tuzo hiyo mjini Strasbourg, Ufaransa. Ni tuzo inayotolewa kila mwaka tangu mwaka 1988 na ina thamani ya Euro 50,000.
Mukwege mwenye umri wa miaka 59 anasema kwamba anaifanya kazi yake ya udaktari kwa moyo wote. "Baba yangu alikuwa mchungaji na amenipa kipaji cha kuwahudumia wengine. Kwangu ilikuwa jambo la kawaida kabisa na nilisema itakuwa vizuri nikiiendeleza kazi hii," alisema Mukwege.
Mtetezi wa haki za wanawake
Baada ya kumaliza masomo yake ya udaktari nchini Burundi, Mukwege alifanya kazi katika hospitali moja mkoani Kivu ya Kusini. Alishangaa kuona kuwa wanawake wengi walikufa wakati walipokuwa wanajifungua. Hivyo akaamua kujikita zaidi katika udaktari wa wanawake. Alikwenda kusoma Ufaransa na baada ya kuhitimu akarudi nchini mwake. Ilikuwa miaka ya 1990 na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilikuwa vimetanda Kongo. Maaskari na waasi walikuwa wanabaka wanawake. Mukwege alifungua hospitali ya Panzi mjini Bukavu na kuamua kuwahudumia haswa wanawake hao, wahanga wa ubakaji.
Mbali na kuwa daktari wa wanawake, Mukwege pia ni mtetezi wa haki za wanawake. Lakini anakiri kwamba udhalilishaji wa wasichana na akina mama hauwezi kuisha bila shinikizo la kimataifa. "Haitasaidia kuwapeleka waasi jela. Ukimfunga mmoja leo, kesho anazaliwa mwingine," anaamini daktari huyo.
Kwa sehemu fulani, daktari Mukwege anahatarisha maisha yake kwa kazi anayofanya. Miaka miwili iliyopita, watu wasiojulikana waliivamia nyumba yake wakiwa wamebeba bunduki. Kwa bahati nzuri, yeye na familia yake waliweza kutoroka. Kwa muda wa miezi mitatu waliishi Ulaya wakihofia maisha yao. Lakini mashirika ya wanawake nchini Kongo yaliahidi kumsaidia na yalijitolea hata kumpatia walinzi. Mukwege sasa amerudi Kongo na anaishi ndani ya hospitali yake, mahali anapojisikia salama zaidi.
Mwandishi: Philip Sandner
Tafsiri: Elizabeth Shoo
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman