Daktari wa zamani wa Rwanda apandishwa mahakamani Paris
1 Oktoba 2024Rwamucyo, mwenye umri wa miaka 65, anatuhumiwa kuhusika kuzisaidia mamlaka za nchi yake katika kuendeleza propaganda dhidi ya jamii ya Watutsi pamoja na kushiriki kwenye mauaji ya watu wengi katika juhudi za kuharibu ushahidi wa mauaji ya kimbari.
Daktari huyo wa zamani anashtakiwa kwa mauaji, kushirikiana na wauwaji, uhalifu dhidi ya ubinaadamu, kushiriki kwenye uhalifu dhidi ya ubinaadamu pamoja na kula njama ya kuandaa matukio hayo ya uhalifu.
Soma zaidi: Rwanda: Kumbukumbu ya miaka 27 tangu kutokea mauaji ya kimbari
Endapo atakutwa na hatia, huenda akakabiliwa na kifungo cha maisha jela.
Wakili wake, Philippe Meilhac, amesema mteja wake amekanusha kuhusika na makosa ya aina yoyote na kwamba tuhuma zinazomuandama zinatokana na hatua yake ya kuipinga serikali ya sasa nchini Rwanda.
Takribani mashahidi 60 wanatarajiwa kutoa ushahidi mbele ya mahakama katika kesi hiyo itakayoendelea hadi Oktoba 29.