1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

290709 China Minderheiten

Charo Josephat29 Julai 2009

Makundi madogo ya China yabanwa na utawala wa China

Kiongozi wa kidini wa Tibet Dalai LamaPicha: AP

Kiongozi wa kidini wa jimbo la Tibet, Dalai Lama, yuko mjini Frankfurt hapa Ujerumani. Kiongozi huyo mbali na kuzuru Ujerumani kama kiongozi wa dini ya Budha amekuja pia kulifuatilia swala la uhuru wa jimbo la Tibet linalojaribu kujikwamua kutokana na udhibiti wa China. Mwezi uliopita wa Julai kulizuka machafuko kati ya Wachina wa kabila la Han na kabila la Uighur katika jimbo la Xinjiang, kaskazini magharibi mwa China, ambapo watu takriban 200 waliuwawa.

Nchini China makundi 55 ya watu wa makabila madogo yanaoongozwa na sheria za kujitawala wenyewe. Ukweli wa mambo lakini ni mwingine kabisa. Mara kwa mara watu wa makundi madogo nchini China hawana haki halisi.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa jukwaa la kiuchumi kati ya Marekani na China, mjini Washington Jumatatu wiki hii, rais wa Marekani, Barack Obama, alisisitiza umuhimu wa kuheshimu utamaduni na uhuru wa kidini wa makundi madogo, ikiwemo pia nchini China.

"Tunaamini pia kuwa dini na utamaduni wa watu wote lazima uheshimiwe na ulindwe. Na kwamba watu wote wanatakiwa kuwa na uhuru wa kutoa maoni yao. Na hiyo inayajumulisha makundi madogo ya kikabilia na kidini nchini China."

Rais wa Marekani Barack ObamaPicha: AP

Jinsi China inavyowashughulikia raia wa jimbo la Tibet na Waughur mara kwa mara hutoa mianya ya ukosoaji kutoka kwa wanaharakati wa makundi ya kutetea haki za binadamu. Mbali na makundi haya madogo yanayojulikana sana nchini China, kunayo makundi mengine 53 madogo. Kubwa ni kabila la Zhuang lenye watu milioni 16 na dogo kabisa ni kundi la Lhoba lenye watu wapatao 3,000 ambao wanaoishi katika jimbo la Tibet. Maeneo yanayokaliwa na makabila madogo yanajumulisha thuluhti mbili ya ardhi yote ya China. Mara nyingi maeneo haya yana utajiri wa malighafi muhimu au yanapakana na maeneo yenye umuhimu mkubwa kwa utawala wa China.

Nchini China kuna maeneo matano makubwa yanayojitawala na majimbo zaidi ya 100 yanayojitawala yenyewe. Katika miaka ya 1980 haki za watu wa makundi madogo wanaoishi katika maeneo hayo ziliimarishwa rasmi. Mageuzi ya kikatiba na sheria za utawala wa maeneo yanayojitawala yalifanyika mnamo mwaka 1984 na kuwaongezea haki watu wa makabila madogo nchini China. Orodha ya haki hizo inaonekana ya kuvutia na kuridhisha, kama anavyoeleza bwana Gardner Bovingdon, mtafiti wa Marekani anayefanya utafiti kuhusu kabila la Waighur nchini China.

"Katiba na sheria za kujitawala za mwaka 1984 zinaunga mkono haki ya kutumia na kuendeleza lugha, haki ya kuwa na wanachama wa makundi madogo kushikilia nyadhifa muhimu katika utawala wa mitaa. Haki ya kulinda tamaduni zao, haki ya uhuru wa kidini na haki ya kudurusu, kurekebisha na hata kukataa sheria za kitaifa ambazo hazifai kwa tamaduni."

Wanawake waislamu wa kabila la Waughur huko Urumqi nchini ChinaPicha: dpa

Licha ya mageuzi ya kikatiba na sheria kuwapa haki zaidi watu wa makabila madogo nchini China, ukweli wa mambo ni mwingine kabisa. Haki hizi hazina thamani kubwa, anasema Björn Alpermann, mtaalam wa lugha na utamaduni wa Kichina, kutoka mjini Würzburg hapa Ujerumani.

"Haki za maeneo ya makabila madogo yanayotajwa kuwa yanajitawala zimebaki kwenye karatasi tu. Nyingi ya haki hizo bado hazijatekelezwa. Na hii ni kwa sababu kwa kiasi kikubwa pia katika maeneo haya chama cha kikomunisti cha China kina ushawishi mkubwa wa kisiasa na kinadhibiti utekelezaji wa haki hizo."

Chama cha kikomunisti kinaweza kufanya hivyo kwa sababu serikali na chama nchini China ni vitu visivyoweza kutengana. Chama hicho hakiko chini ya sheria. Wakereketwa wa chama wana mamlaka ya kutekeleza amri za serikali. Wanaweza kuvunja sheria. Utawala wa chama uko juu ya utawala wa serikali na taasisi zake, ndio maana gavana wa jimbo anaweza kuwa mkaazi wa eneo hilo. Nafasi muhimu ya katibu mkuu wa chama cha Komunisti hushikiliwa na Mchina wa kabila la Han, kwa hiyo uamuzi kuhusu maswala tete yanayoyahusu makabila madogo hayatiliwi maanani. Pia makabila madogo hayana ushawishi mkubwa dhidi ya maeneo yao kuvamiwa na kukaliwa na Wachina wa kabila la Han.

Akiwa ziarani hapa Ujeruamni, bila shaka kiongozi wa kidni wa Tibet, Dalai Lama, anakabiliwa na kibarua kigumu kuhakikisha Watibet wanatendewa haki.

Mwandishi:Matthias von Hein /ZR/Josephat Charo

Mhariri:M.Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW