1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dalili za kupungua makali mzozo wa Korea magazetini

Oumilkheir Hamidou
7 Machi 2018

Uwezekano wa kukutana viongozi wa Korea mbili, mzozo wa Afghanistan , na uhusiano kati ya Ujerumani na Uturuki ni miongoni mwa mada magazetini .

Nordkorea Kim Jong Un spricht mit südkoreanischer Delegation
Picha: Reuters/Yonhap

Tunaanzia katika raasi ya Korea ambako matumaini yanaanza kuchomoza , yakiashiria kupungua makali mvutano kati ya Korea mbili. Hata hivyo mhariri wa gazeti la "Badische Zeitung" anashuku na kuhoji: "Mengi yanaonyesha kwamba Korea ya kaskazini inataka kwa mara nyengine tena kuuchezea ulimwengu. Bila ya shaka Kim anabisha hodi katika mlango ambao pengine ni rahisi kufunguliwa. Mikutano miwili ya kilele imeshawahi kuitishwa kati ya Korea mbili na kuitikwa kwa moyo mkunjufu na Korea ya Kusini. Na kila mara wameondoka patupu-Korea ya Kusini inagharimia na Korea ya Kaskazi inaendelea kutengeneza mabomu.."

 Ugonjwa usiokua na dawa wa Afghanistan

Tunasalia huko huko barani Asia ambako mzozo wa Afghanistan unalinganishwa na ugonjwa usiokuwa na dawa. Juhudi za amani kila mara zinashindwa, na kwa namna hiyo kuzidi kuwalazimisha vijana kuipa kisogo nchini hiyo . Gazeti la "Rheinpfalz" linaandika: "Tangu zama za zama Afghanistan ni nchi ya vurugu. Iko mbali kabisa kugeuka nchi ya kimambo leo yenye kufuata mfumo wa kidemokrasia kama zinavyopendelea nchi za magharibi. Imegawika kati ya makundi makubwa ya kikabila ya Pashtun,Tadjiki, Uzbeki na Hazara na kujitenganisha miongoni mwa maelfu ya  koo zinazohasimiana. Wote hao hawana hamu ya kutaka kushirikiana kwasababu kwao wao eno "utiifu" ni sawa na kitu kinachonunulika kisichokuwa na thamani kubwa. Hali hiyo ndio chanzo cha mikururo ya wakimbizi wa kiuchumi ambacho bado watu wanashindwa kukielewa nchini Ujerumani."

Uturuki kusawazisha uhusiano pamoja na Ujerumani

Ujerumani na Uturuki zinajitahidi kupunguza mivutano iliyozidi makali tangu njama ya mapinduzi iliyoshindwa msimu wa kiangazi mwaka 2016. Gazeti la "Rhein-Zeitung linazungumzia mipaka ambayo Ujerumani haistahili kuikiuka. Gazeti linaendelea kuandika: "Berlin isikubali hata kidogo kunasa katika mtego wa kibiashara wa Uturuki. Waziri wa mambo ya nchi za nje Sigmar Gabriel alihakikisha Ujerumani haikuahidi itaipatia Uturuki vifaru kwaajili ya vita vyake dhidi ya wakurd kaskazini mwa Syria, ili badala yake mwandishi habari Deniz Yücel aachiwe huru. Tunataraji atatekeleza alichokiahidi. Uturuki inataka pia kuona onyo dhidi  ya kuitembelea nchi hiyo linaondoshwa. Waziri wa mambo ya nchi za nje Mevlut Cavosoglu hakulificha hilo. Uturuki inataka kurejesha uhusiano wa kawaida na Ujerumani kwasababu za kiuchumi. Kwasababu Ankara inatambua: Njia ya kuelekea Ulaya inapitia Berlin."

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri:Yusuf Saumu

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW