DAMASCUS: Chama cha Hamas chaikosoa Marekani
20 Februari 2007Naibu kiongozi wa chama cha Hamas, Moussa Abu Marzouk, ameikosoa vikali Marekani kwa kumbinya rais wa mamlaka ya Palestina, Mahmoud Abbas, ayakatae makubaliano ya kuunda serikali ya umoja wa taifa yaliyofikiwa baina ya chama cha Hamas na Fatah.
Marzouk aliuambia mkutano uliofanyika kwenye kambi ya wakimbizi ya Yarmouk kusini mwa Damascus nchini Syria kwamba sera ya Marekani imekita katika kupalilia uhasama miongoni mwa watu na mataifa ya eneo zima la Mashariki ya Kati.
Mkutano huo ulifanyika kupinga hatua ya Israel kuchimba kiwanja cha mahala patakatifu pa Haram al Sharif mjini Jerusalem.
Waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani Condoleezza Rice alisema mjini Ramallah Jumapili iliyopita kwamba Marekani itaamua kuhusu uhusiano wake na serikali mpya ya Palestina mara tu itakapoundwa.