1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DAMASCUS: Maelfu ya wasyria waandamana kuipinga ripoti ya umoja wa mataifa juu ya kifo cha Hariri

24 Oktoba 2005

Maelfu ya raia wa Syria wamefanya maandamano kuiunga mkono serikali yao huku baraza la usalama la umoja wa mataifa likijianda kuijadili ripoti ya mauji ya waziri mkuu wa zamani wa Lebanon, Rafik Hariri, hapo kesho.

Mamia ya wanafunzi waliandamana hadi katikati ya mji wa Damascus huku wakipiga kelele wakisema Mungu, Syria na Bashar. Walibeba bendera ya Syria na mabango yaliyokuwa na maandishi ya kuipinga ripoti ya hakimu wa Ujerumani, Detlev Mehlis. Waandamanaji hao wameapa kumlinda rais wao Bashar al-Assad hata ikiwa watalazimika kuimwaga damu au kupoteza uhai wao.

Wakati huo huo, waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, Bi Condoleezza Rice, amesema Marekani ina matumaini kwamba jamii ya kimataifa itaichukulia hatua Syria kwa kutajwa katika ripoti ya umoja wa mataifa juu ya uchunguzi wa kifo cha Hariri. Amesema azimio la 1559 la umoja wa mataifa lililoifanya Syria kuwaondoa wanajeshi wake kutoka Lebanon, linadhihirisha kwamba Syria inaheshimu amri ya jumuiya ya kimataifa.

Amesisitiza kwamba sio Marekani iliyo na jukumu la kuiadhibu Syria ila jamii ya kimataifa, na ikiwa ulimwengu utaungana pamoja bila shaka kutapatikana njia muafaka za kukabiliana na matatizo ya Syria. Bi Rice anataka athari za ripoti hiyo iliyowasilishwa na mchunguzi wa Ujerumani, Detlev Mehlis, zijadiliwe katika ngazi ya kimataifa.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW