1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dani Alves atuhumiwa kwa kumnyanyasa kingono mwanamke

20 Januari 2023

Mlinzi wa timu ya taifa ya Brazil Dani Alves anashikiliwa kizuizini Uhispania kwa madai ya kumnyanyasa kingono mwanamke mmoja katika klabu ya usiku ya Barcelona mwezi Disemba, hii ikiwa ni kulingana na jeshi la polisi.

Brasilien Der Fußballspieler Dani Alves
Picha: ULISES RUIZ/AFP

Dani Alves, 39 ambaye aliitwa na polisi ya Barcelona na kukamatwa anasubiri kuhojiwa na jaji, amesema msemaji wa jeshi la polisi jimbo la Catalonia, wakati vyombo vya habari vya Uhispania vikiarifu kwamba mchezaji huyo atahojiwa na polisi kuhusiana na madai hayo kupitia mawakili wake. Mwanamke huyo aliwasilisha madai hayo kituoni mnamo Januari 2, akisema Alves alimpapasa bila ya idhini yake, jeshi hilo limesema.

Vyombo vya habari vya nchini humo vimesema Alves alifanya vitendo hivyo Disemba 30 kuamkia 31, katika klabu ya usiku ambayo ni maarufu mno iliyoko Barcelona na baadae msichana huyo aliwaarifu walinzi wa klabu ambao waliitumia kanuni ya halmashauri ya jiji kuhusiana na unyanyasaji wa kingono dhidi ya vitendo vya Alves.

Dani Alves anaonekana akiruka juu wakati timu yake ilipokwaana na Mexico katika michuano ya Olimpiki ya soka kwa wanaume huko Tokyo, mwaka 2020.Picha: Edgar Su/REUTERS

Mwenyewe amethibitisha kwamba alikuwepo kwa klabu hiyo ya usiku, lakini anakana kufanya jambo lolote ovu, na mapema mwezi huu alikiambia kituo binafsi cha televisheni cha Antena 3 kwamba hakuwahi hata kumuona mwanamke huyo. "Nilikuwepo pale na wenzangu kadhaa tukijivinjari. Kila mtu anajua kuwa napenda kucheza muziki na kufurahi, lakini bila ya kuvuruga wala kuingilia starehe za wengine," aliongeza mchezaji huyo wa zamani wa Barcelona, Juventus na Paris Saint-Germain.

Mkewe Joana Sanz amekiambia kituo hicho cha televisheni cha Antenna 3 kwenye mahojiano ya Januari 9 kwamba mumewe alikwenda kupata chakula cha jioni na wenzake. Akasema baada ya hapo alikwenda kucheza muziki na hakufanya jingine lolote. "Hakuna lolote baya lililotokea...namjua namna anavyojiheshimu," aliongeza.

Alves ambaye sasa anakipiga na Pumas UNAM ya Mexico alikuwa likizoni Barcelona baada ya kushiriki michuano ya Kombe la Dunia huko Qatar akiwa na timu ya taifa ya Brazil.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW