Daniel Noboa ashinda uchaguzi wa urais nchini Equador
16 Oktoba 2023Baada ya asilimia 93 ya kura kuhesabiwa, Noboa alikuwa mbele kwa asilimia 52 huku Gonzalez akiwa wa pili kwa asilimia 48.
Baraza la uchaguzi nchini humo limesema kulingana na kura zilizokwisha hesabika, matokeo hayo hayawezi yakabadilika.
Noboa ameahidi kurudisha amani katika nchi hiyo iliyovurugwa na vita vya umwagaji damu vya magenge ya ulanguzi mihadarati.
Gonzalez amekubali kushindwa na amempongeza Noboa kwa ushindi wake.
Amesema hayo alipokuwa akizungumza na wafuasi wake mjini Quito.
Wagombea hao wawili walishiriki kura ya marudio baada ya kuchukua nafasi ya kwanza na pili mbele ya wagombea wengine sita katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa Agosti 22.
Masuala makuu ambayo yanawapa wapiga kura changamoto nchini humo ni pamoja na uchumi ambao umetatizika tangu kutokea kwa janga la COVID-19, ongezeko la uhalifu ikiwemo mauaji na ghasia za magerezani.