Dar Es Salaam. Chama cha CUF kushiriki uchaguzi wa taifa.
6 Novemba 2005Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania kimesema kuwa kitashiriki katika uchaguzi mkuu wa taifa unaokuja, lakini chama hicho kitafanya maandamano makubwa iwapo maafisa hawatafanya uchunguzi wa madai ya udanganyifu katika uchaguzi wa wiki iliyopita katika kisiwa cha Zanzibar.
Chama cha upinzani cha Civic United Front , CUF kimesema kuwa chama tawala kimefanya udanganyifu mkubwa katika uchaguzi wa Oktoba 30 katika kisiwa cha Zanzibar , kisiwa kilichojiunga na Tanganyika mwaka 1964 na kuunda jamhuri ya muungano wa Tanzania .
Viongozi wa chama hicho wakikutana katika mji wa kibiashara wa Dar es Salaam wamerudia kukataa kwao matokeo ya uchaguzi na kuongeza kuwa hawamtambui rais wa Zanzibar Amani Abeid Karume. Chama hicho pia hakitashirikiana na serikali yake, msemaji wa chama hicho cha upinzani Ismail Jussa amesema .
Lakini wabunge waliochaguliwa kwa ajili ya baraza la wawakilishi Zanzibar wataingia bungeni , Jussa ameliambia shirika la habari la Associated Press.