Dar Es Salaam. Ghasia zazuka katika kampeni za uchaguzi.
24 Septemba 2005Zaidi ya watu 20 wamejeruhiwa na wengine 14 wamekamatwa na polisi wakati waungaji mkono wa vyama hasimu vya kisiasa walipopambana kaskazini mwa Tanzania baada ya mikutano ya kampeni kabla ya uchaguzi mkuu mwezi ujao.
Polisi na watu walioshuhudia wamesema jana kuwa ghasia hizo zilitokea jioni ya Alhamis katika mji ulioko kaskazini magharibi wa Bukoba kiasi cha kilometa 1,400 kutoka mji mkuu Dar Es Salaam , kati ya waungaji mkono wa chama tawala CCM na kundi la chama kikuu cha upinzani.
Afisa mwandamizi wa polisi mjini Bukoba Gregory Puka amesema kuwa wale waliohusika walikuwa wakirushiana mawe na watu 14 walikamatwa kwa kuhusika na tukio hilo.
Watu walioshuhudia wamesema kuwa mapambano hayo yalikuwa kati ya waungaji mkono wa chama tawala CCM na chama cha upinzani cha CUF, ambao ndio wapinzani wakuu katika uchaguzi mkuu utakaofanyika hapo Oktoba 30.
Uhasama mkubwa kati ya waungaji mkono wa vyama hivyo ulikuwa kwa muda mrefu ukitokea katika kisiwa chenye madaraka yake ya ndani cha Zanzibar, ambako hali ya wasi wasi inazidi kupanda na mapambano kadha ya ghasia yameripotiwa katika miezi ya hivi karibuni.