DAR ES SALAAM: Mkutano wa SADC wajadili migogoro ya Zimbabwe
29 Machi 2007Viongozi wa nchi za kusini mwa Afrika hii leo wanakutana na rais Robert Mugabe wa Zimbabwe kuijadili migogoro ya nchi yake inayozidi kushika kasi.Mkutano wa dharura wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika-SADC ulianza siku ya Jumatano chini ya uongozi wa rais Jakaya Kikwete wa Tanzania mjini Dar es Salaam.Kwa upande mwingine Afrika ya Kusini kwa mara ya kwanza imeikosoa vikali serikali ya Zimbabwe.Naibu waziri wa nje wa Afrika ya Kusini,Sue van der Merwe amesema,serikali ya Afrika ya Kusini inataka kusisitiza wasiwasi wake,masikitiko na kutoridhika kwake kuhusu hatua zilizochukuliwa na polisi kukabiliana na wapinzani nchini Zimbabwe. Amesema,hali ya kisiasa inayokutikana nchini Zimbabwe hivi sasa ni matokeo ya kutofanywa majadiliano.Na hiyo huzidisha migogoro ya kisiasa na uchumi nchini humo aliongezea van der Merwe.Wakati huo huo ripoti zinasema,polisi nchini Zimbabwe ilivamia makao makuu ya chama kikuu cha upinzani MDC na watu 35 walikamatwa ikiwa ni pamoja na kiongozi wa MDC,Morgan Tsvangirai.Lakini vikosi vya usalama vimekanusha habari hiyo na kusema kuwa ni maafisa wengine 10 wa MDC ndio waliokamatwa wakishukiwa kuhusika na miripuko ya bomu iliyotokea hivi karibuni nchini humo.Na Ujerumani iliyoshika wadhifa wa urais katika Umoja wa Ulaya,imetoa wito kwa serikali ya Zimbabwe kuheshimu sheria.Tsvangirai na wanachama darzeni kadhaa wa MDC walikamatwa na kupigwa vibaya sana na polisi kiasi ya majuma mawili yaliyopita.