1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Davos: Kongamano la uchumi wa dunia lamalizika

Zainab Aziz Mhariri: Mohammed Khelef
24 Januari 2020

Mwanaharakati kijana wa kutetea ulinzi wa mazingira, Greta Thunberg, amelalamika juu ya kupuuzwa kwa miito ya kuyataka makampuni makubwa kuacha kuwekeza katika uzalishaji wa nishati za mafuta, gesi na makaa ya mawe.

Schweiz Weltwirtschaftsforum 2020 in Davos
Picha: Reuters/D. Balibouse

Mwanaharakati huyo amesema katika siku ya mwisho ya kongamano hilo kwamba miito kadhaa imetolewa lakini imepuuzwa kabisa. Hata hivyo ameeleza kuwa, hakutegemea lingine. Msichana huyo ambaye alikuwa nyota kwenye mkutano huo wa 50 wa masuala ya uchumi wa dunia alikuwa na mvuto mkubwa kwa washiriki wengine ikiwa pamoja na waziri wa fedha wa Marekani Steven Mnuchin aliyembeza msichana huyo kwa kumwambia aende kusomea mambo ya uchumi kwanza. Dada huyo amejibu kwa kusema wanaharakati wa ulinzi wa mazingira wanakosolewa wakati wote, lakini amesema wakizijali shutuma hizo hawataweza kufanya lolote.

Malumbano baina  ya Thunberg na waziri wa Marekani yanabainisha mivutano iliyopo juu ya suala la mabadiliko ya tabia nchi kwenye kongamano la mjini Davos ambapo kampuni na serikali zilibanwa na kutakiwa zichukue hatua mara moja ili kukabiliana na ongezeko la joto duniani.

Waziri wa fedha wa Marekani Steven Mnuchin amesema haamini iwapo imebakia miaka michache tu ili kuweza kuepusha maafa ya mabadiliko ya tabia nchi. Waziri huyo amesema yapo masuala mengine yanayowatishia binadamu, kama vile magonjwa na kuenea kwa silaha za nyuklia.

Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: Reuters/U. Betkas

Hata hivyo Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amemtetea mwanaharakati wa mazingira binti mwenye umri mdogo GretaThunberg. Akizungumza mjini Davos kansela Merkel amesema maazimizo yaliyopitishwa  kwenye mkutano wa mjini Paris juu ya ulinzi wa mazingira ni muhimu sana na yanapaswa  kutekelezwa.

Marekani imejitoa kwenye mkataba wa Paris uliofikiwa mnamo mwaka 2015. kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema inapasa viongozi wayasikilize malalamiko ya vijana kwa mzatamo chanya. Katika hotuba yake kiongozi wa Ujerumani amesema anatumai lengo la kuondokana kabisa na gesi zinazoharibu mazingira litafikiwa sambamba na lile la kuleta mapinduzi ya kijiditali duniani.

Merkel amesema mabadiliko hayo maana yake ni kuachana kabisa na mtindo wa maisha tuliouzoea hadi sasa katika enzi ya viwanda lakini ameeleza matumaini yake kwamba mengi yanaweza kutekelezwa katika kipindi cha miaka 30 ijayo ikiwa misingi ya uzalishaji wa nishati itabadilishwa kwa ukamilifu.

Vyanzo: RTRE/AFP

 

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW