1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dbeibah alikosoa bunge la Libya kumchagua mrithi wake

11 Februari 2022

Waziri Mkuu wa serikali ya mpito ya Libya, Abdulhamid al-Dbeibah, amesema hatua ya bunge kuichagua serikali mpya ni jaribio jingine la kuingia Tripoli kwa nguvu.

Ägypten Kairo | Libyscher Premierminister Abdul Hamid Mohammed Dbeibah
Picha: Hazem Ahmed/AP Photo/picture alliance

Akizungumza Ijumaa katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Al Ahrar, Dbeibah amesema bado anakataa jaribio lolote lile la kuwaingiza Walibya katika vita vipya. Hata hivyo, ameahidi kuandaa mpango mpya wa kuutatua mzozo wa kisiasa nchini Libya na amesema anaweza kuutangaza mpango wa serikali yake katika siku zijazo.

Kiongozi huyo wa serikali ya mpito ya Umoja wa Kitaifa ya Libya, GNU ambaye jana alinusurika katika jaribio la kuuawa, amesema mpango huo utahusisha kuandaa sheria mpya ya uchaguzi. Amesema muswada utawasilishwa katika Baraza la Wawakilishi na kisha utapelekwa kwenye Baraza la Rais ili uweze kupitishwa.

Kutogombea uchaguzi wa urais

Dbeibah pia ametangaza nia yake ya kutogombea kwenye uchaguzi wa urais kwa lengo la kuufanikisha mpango huo, ingawa ameapa kubakia madarakani hadi hapo uchaguzi utakapofanyika.

Kwa upande wake Waziri Mkuu mpya wa Libya aliyechaguliwa Alhamisi na bunge kuchukua nafasi ya Dbeibah, Fathi Bashagha, amewasili katika mji mkuu wa Libya, Tripoli. Bashagha aliyekuwa waziri wa zamani wa mambo ya ndani ya Libya, ameishukuru serikali ya GNU kwa juhudi zake na amesema anatarajia ushirikiano mzuri na kufanya kazi pamoja nayo.

''Serikali ijayo itakuwa serikali ya wote na ya kila mtu, na tunatarajia kushirikiana na wote bila ubaguzi. Siku zote tutashirikiana na Baraza la Wawakilishi na Baraza la Kitaifa na serikali haiwezi kufanikiwa bila ushirikiano. Hakuna haja ya chuki, kulipiza kisasi wala dhuluma. Tuko tayari kufungua ukurasa mpya wa kitaifa unaozingatia amani na upendo,'' alisisitiza Bashagha.

Waziri Mkuu mpya wa Libya aliyechaguliwa na bunge Fathi Bashagha, Picha: Hazem Turkia/AA/picture alliance

Bashagha ameishukuru serikali inayoongozwa na Dbeibah ambayo amesema ilichukua madaraka na kutekeleza majukumu yake katika kipindi kigumu.

Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa umesema utaendelea kumuunga mkono Dbeibah, licha ya bunge kumchagua Bashagha, kuchukua nafasi yake. Umoja huo umesema unaendelea kumtambua Dbeibah kama waziri mkuu wa mpito.

Juhudi za kimataifa mashakani

Serikali ya GNU inayoongozwa na Dbeibah ilianzishwa mwaka uliopita kupitia mchakato uliosimamiwa na Umoja wa Mataifa. Wabunge wamesisitiza kuwa mamlaka yake yamekamilika, kwani alitakiwa kukabidhi madaraka baada ya uchaguzi wa Desemba.

Bunge la Libya ambalo lilichaguliwa mwaka 2014 na likiegemea zaidi vikosi vya mashariki wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe, limesema limechukua uamuzi huo kutokana na Dbeibah kushindwa kuitisha uchaguzi wa kitaifa uliokuwa umepangwa kufanyika mwezi Desemba, suala ambalo walikuwa wamekubaliana chini ya mchakato wa amani uliosimamiwa na Umoja wa Mataifa.

Kucheleweshwa kwa uchaguzi huo ni pigo kwa juhudi za kimataifa za kuumaliza mzozo wa muongo mmoja kwenye taifa hilo la Afrika Kaskazini lenye utajiri wa mafuta.

(AP, AFP, Reuters)