1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

De La Fuente: Ndio mwanzo mkoko waalika maua Uhispania

19 Juni 2023

Uhispania Jumapili waliubeba ubingwa wa kombe la UEFA Nations League baada ya kuishinda Croatia katika fainali 5-4 kupitia mikwaju ya penalti.

UEFA Nations League Finale Spanien Kroatien
Picha: Martin Meissner/AP Photo

Kocha wa Uhispania Luis de la Fuente baada ya kuipa timu yake kombe la kwanza la kimataifa baada ya zaidi ya mwongo mmoja amesema kwamba huu ndio mwanzo wa mkoko kualika maua kwa timu yake yenye vijana.

"Matokeo hayajalishi, hata kama hatungeshinda ningekuwa na furaha sana kwasababu wamejitahidi sana kujaribu kufunga goli. Bila shaka ushindi unafanya kila kitu kuwa bora zaidi kwasababu unaongeza kule kumeta meta nilikokuwa nazungumzia jana. Kwa hiyo sote tuna furaha, vijana hawa wanastahili tu kujitahidi waufikie uwezo wao kwasababu wanaweza. Natarajia mengi zaidi kutoka kwao katika miaka ijayo. Tutarajie furaha nyingi zaidi kutoka kwa kikundi hiki cha wachezaji," alisema de la Fuente.

Modric afanya uamuzi ila apiga kimya

Kwengineko kushindwa kwa Croatia kulimaanisha kwamba wanapoteza fainali ya pili ya kimataifa baada ya Kombe la Dunia waliposhindwa na Ufaransa nchini Urusi. Lakini kitakachowahuzunisha pakubwa mashabiki wa Croatia ni kwamba huenda hiyo ya jana ikawa ndiyo mechi ya mwisho ya nahodha wao Luka Modric.

Luka ModricPicha: Kenzo Tribouillard/AFP

Modric alipohojiwa baada ya mechi hiyo alisema kwamba ameshafanya uamuzi kuhusiana na mustakabali wake katika timu ya taifa ila hatofungua mdogo kuuzungumzia kwa sasa. Kocha wake Zlatko Dalic alikuwa na haya ya kusema.

"Tunahitaji kupumzika kutokana na yote haya, tunahitaji kuacha vumbi litulie tuyafikirie yote. Kulikuwa na wasiwasi na vilio vingi ila Modric alicheza mchezo mzuri. Alikimbia kwa dakika 120 kwa mara ya pili katika kipindi cha siku nne. Ningependa Luka asalie. Ni mchezaji muhimu sana na natarajia kwamba atasalia nasi kwa muda mrefu zaidi," alisema Dalic.

Chanzo: Jacob Safari/AP/DPA