1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Deby ashinda uchaguzi mkuu

10 Mei 2024

Kiongozi wa kijeshi nchini Chad Mahamat Idriss Deby Itno ametangazwa mshindi wa uchaguzi wa rais uliofanyika Mei 6, lakini mpinzani wake mkuu anayapinga matokeo hayo yaliyotangazwa na tume ya uchaguzi

Chad
Kiongozi wa kijeshi nchini Chad Mahamat Idriss Deby Itno ametangazwa mshindi wa uchaguzi wa rais uliofanyika Mei 6Picha: Blaise Dariustone/DW

Tuelekee huko nchini Chad ambapo kiongozi wa kijeshi nchini humo Mahamat Idriss Deby Itno ametangazwa mshindi wa uchaguzi wa rais uliofanyika Mei 6, lakini mpinzani wake mkuu anayapinga matokeo hayo yaliyotangazwa na tume ya uchaguzi. Ushindi huo wa Deby utarefusha utawala wa familia yake ambayo imekuwepo madarakani kwa miongo kadhaa sasa. 

Soma zaidi. Idriss Deby Itno atangazwa kushinda uchaguzi Chad
Kura zilizopigwa siku ya Jumatatu ya wiki hii zililenga kuumaliza utawala wa miaka mitatu wa kijeshi katika nchi hiyo ya kanda ya Sahel iliyopo kwenye mapambano na makundi ya itikadi kali za dini ya kiislamu.

Kiongozi wa kijeshi nchini Chad Mahamat Deby akishiriki katika zoezi la kupiga kuraPicha: Mouta/AP Photo/picture alliance

Tume ya taifa ya uchaguzi, imesema Deby ameshinda uchaguzi huo kwa asilimia 61, akimshinda mpinzani wake na aliyekuwa waziri mkuu Succes Masra aliyeshika nafasi ya pili na kupata asilimia 18 ya kura. Matokeo hayo yanasubiri kuidhinishwa na Baraza la kikatiba.

Ushindi wa Deby sio jambo la kushangaza

Kwa wafuatiliaji wa uchaguzi huo wanasema kuwa ushindi wa Mahamat Idriss Deby Itno katika duru ya kwanza ya uchaguzi sio jambo la kushangaza kwao, Akiyaelezea matokeo ya uchaguzi huo Remadji Hoinathy ambaye mchambuzi wa kisiasa za nchini Chad amesema

 "Mahamat Idriss Déby kuchaguliwa kwa kura nyingi ilikuwa hali iliyotarajiwa kwa sababu tangu kuanza kwa mchakato huu na jinsi chombo kinachosimamia usimamizi wa uchaguzi kilivyoundwa na watendaji wa kisiasa ilikuwa ni wazi kuwa wako upande mmoja wa kisiasa na ule waliotangaza matokeo ya urais, na kwa hivyo uanzishwaji huo ulikuwa hautoi nafasi kwa wagombea wengine''.

Soma zaidi. IRC: Mamilioni wakabiliwa na uhaba wa chakula Sahel

Kwa upande mwingine yapo pia maoni yaliyotolewa na waharakati wa haki za binadamu wakidai kuwa  Ufaransa ambayo ni mshirika mkubwa wa Chad ipo nyuma ya ushindi wa Deby. Huyu ni Jean-Bosco, Mwanaharakati wa haki za binadamu.

Mahamat Idris Deby ametangazwa kushinda uchaguzi mkuu nchini Chad katika duru ya kwanzaPicha: Blaise Dariustone/DW

"Matokeo haya yanaweza kuwa ya kushangaza kwa wale ambao hawajaelewa mchezo wa kisiasa ambao umekuwa ukichezwa tangu kipindi cha mpito, Ufaransa imeamua kumpitisha rais huyu wa mpito ili kutopoteza ushawishi wake nchini Chad. Na pia tumefahamu kupitia makubaliano ya Kinshasa (kuhusu serikali ya mpito ya Chad) kuna michezo ya kisiasa ambayo haijawekwa wazi mbele ya umma ameeleza Jean Bosco.

Masra hayaungi mkono matokeo ya tume

Saa moja kabla ya kutangazwa kwa matokeo hayo yaliyompa ushindi Derby aliyekuwa Waziri Mkuu wake Succes Masra aliyapinga matokeo hayo na kuwataka wananchi wa Chad kuudai ushindi wao.

Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Chad Succes Masra ameyapiga matokeo yaliyotangazwa na tumePicha: Issouf Sanogo/AFP

Kwa mara nyingine, Mchambuzi wa masula ya kisiasa Remadji Hoinathy anatoa wito wa kufanyika kwa mazungumzo ili kupeusha umwagaji wa damu nchini Chad.

Soma zaidi. Wachad wapiga kura kuhitimisha utawala wa kijeshi

"Tupo katika hali ambayo kunaweza kuwa na mvutano wa uso kwa uso barabarani kati ya wananchi na polisi hali ambayo inaweza kuishia kwenye umwagaji damu tena.Upatanishi wa dhati tu kitu pekee kinachoweza kuepusha hili na  ni muhimu kwamba wote wahusika wanaohusika na uchaguzi wa Chad kuelewa kuwa umefika wakati sasa kwao kuchukua jukumu muhimu sana katika kuepusha hali ya umwagaji damu tena nchini Chad'' amesema Remadji.

Hata hivyo, muda mfupi baada ya matokeo kutangazwa milio ya bunduki ilisikika katika mitaa ya mji mkuu wa N'Djamena katika kusherehekea ushindi wa Deby na kuwazuia waandamanaji kukusanyika.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW