Denmark yatafuta muafaka EU kupeleka waomba hifadhi nje
25 Januari 2023Waziri wa uhamiaji wa Denmark Kaare Dybvad amesema nchi yake inanuia kufanya kazi na mataifa mengine ya Ulaya, kuwapeleka waomba hifadhi katika vituo vilioko nje ya Ulaya, na imesitisha kwa muda mazungumzo na Rwanda juu ya kufungua taasisi ya waomba hifadhi nchini humo.
Waziri huyo amesema serikali mpya iliyoingia madarakani nchini Denmark bado ina mpango huo lakini mchakato utakaochukuliwa ni tofauti.
Mpango huo wa Denmark uliotangazwa na serikali iliyopita ya chama cha Social Democrats ilitaka watu wanaoomba hifadhi wapelekwe katika vituo vilioko nje ya Ulaya huku maombi yao yakiendelea kufanyiwa kazi.
Sheria iliyopitishwa mwezi Juni mwaka 2021 haikuweka wazi ni nchi gani itakayokuwa na vituo hivyo, lakini ikasema waomba hifadhi watakaa katika maeneo hayo hata baada ya kupewa hifadhi.