1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Denmark yataka kuchukua mali za wakimbizi

Caro Robi23 Desemba 2015

Polisi Denmark imesema haidhani mipango ya kuchukua mali za wahamiaji ili kugharamia mahitaji yao ni jambo linaloweza kutekelezeka. Mapendekezo ya kuchukua mali za wakimbizi yalifichuliwa wiki iliyopita bungeni.

Picha: Reuters/Scanpix/J. Larsen

Mkuu wa muungano wa polisi nchini Denmark Claus Oxfeldt amesema sio kazi ya polisi kutathmini thamani za mali za wakimbizi wanaoingia nchini humo.

Kulingana na mapendekezo hayo yanayoibua utata, hatua hiyo inalenga kutumia mali hizo zitakazochukuliwa ili kugharamia mahitaji ya wakimbizi hao na inazingatiwa kama sehemu ya hatua za kuwavunja moyo wakimbizi zaidi kuelekea Denmark.

Hatua hiyo imefananishwa na ya wanazi

Kitu chochote cha thamani ya zaidi ya euro 400 kitachukiliwa. Hatua hiyo imefananishwa na jinsi wanazi walivyowafanya wayahudi katika vita vya pili vikuu vya dunia walipo wapokonya mali zao.

Wakimbizi wakisubiri treni kutoka Ugiriki kuelekea SerbiaPicha: Getty Images/AFP/R. Atanasovskia

Mkuu huyo wa polisi wa Denmark amesema anapinga pendekezo hilo ambalo linatarajiwa kupigiwa kura bungeni mwezi ujao na huenda likaanza kutekelezwa mwezi Februari.

Mapendekezo hayo hasi kwa wakimbizi yamesababisha kampeini ya mitandaoni ya kukusanya saini za kulishinikiza bunge kutopitisha hatua hiyo.Tayari saini 15,000 zimekusanywa hadi jana.

Mbunge mmoja wa chama tawala nchini Denmark Jens Rhodes amejitoa chamani akipinga pendekezo hilo la kuchukuliwa mali za wakimbizi akisema ni kinyume na maadili anayosimamia.

Imran Shah ambaye ni msemaji wa chama cha Waislamu nchini Denmark ameongeza kusema mkakati huo ni mbinu za kujaribu kubuni kile kinachoweza baadae kugeuka kuwa "mfumo wa jamii ya kubaguana na mtengano."

Lakini chama kinachopinga wahamiaji cha Danish People DPP kinasisitiza nchi hiyo inapaswa kutoa ishara ya kuwazuia wahamiaji kuingia nchini humo.

Msemaji wa DPP Martin Henriksen ameliambia shirika la habari la AFP kuwa wanajribu kuwaambia wahamiaji kama wanapanga kuja Ulaya basi waiepuke Denmark kwasababu wana matatizo na wahamiaji na hawahitaji zaidi.

Mawaziri wa Denmark wamesema mpango huo hautofautiani na masharti waliowekewa raia wa nchi hiyo wanaotakiwa kusema kama akiba yao haipindukii kroner 10,000 kabla hawajaomba kupatiwa msaada wa mafao ya jamii.

Sweden pia haitaki wakimbizi zaidi

Denmark kama nchi jirani, Sweden, inajaribu kuchukua hatua kadha wa kadha kuzuia ongezeko la wahamiaji nchini mwao. Sweden hapo jana ilitangaza inasitisha baadhi ya huduma za reli kuelekea na kutoka Denmark ili kuwazuia wahamiaji kuingia nchini humo.

Kikao cha bunge la DenmarkPicha: AP

Kuanzia mwezi ujao, kampuni za uchukuzi nchini humo zitatozwa faini kama zitawasafirisha abiria wasiokuwa na vitambulisho.

Tangazo hilo la Shirika la reli SJ, linakuja baada ya ombi la serikali ya Sweden kutaka iondolewe kwa muda kutoka makubaliano ya Schengen yanayoziruhusu nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya kusafiri kwa uhuru bila ya visa, ili kuweza kukabiliana na ongezeko la wahamiaji wanaoingia nchini humo wengi wao wakitumia mfumo wa usafiri wa treni kutoka Denmark.

Mwandishi: Caro Robi/http://www.dw.com/en/danish-police-refuse-to-seize-refugee-jewelry-and-cash/a-1893456

Mhariri: Hamidou Oumilkheir

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW