1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Desmond Tutu atimiza miaka 90 ya kuzaliwa

6 Oktoba 2021

Desmond Tutu ambaye anatimiza umri wa miaka 90 Alhamis, bado ni mfano wa kuigwa kwa maadili mema nchini Afrika Kusini. Lakini Askofu huyo amekuwa akizungumza mara chache sana hadharani.

Südafrika Desmond Tutu und Egil Aarvik
Picha: dpa/picture alliance

Pia wakati mwengine hujiona kama yatima kwa kuwakosa watu walioshirikiana nae katika mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi maarufu kama "Apartheid".

Desmond Tutu, aliyestaafu tangu mwaka 2010, anasherehekewa leo kama shujaa alieupinga utawala wa kibaguzi uliochukiwa mno nchini Afrika Kusini. Umri wa wastani nchini humo ni miaka 27, na vijana wengi hawamfahamu vyema mzee Tutu isipokuwa katika vitabu vya shule. Licha ya vizuizi kutokana na covid-19 kupunguzwa, sherehe ya siku ya kuzaliwa ya Askofu hazitarajiwi kuwa za shamra shamra na kwa sehemu kubwa zitafanyika mtandaoni.

Desmond Tutu, anaezoeleka kwa ucheshi wake, ni askofu mkuu wa kwanza mweusi wa Kianglikana nchini Afrika Kusini, anatarajia kuhudhuria ibada iliyoandaliwa mahsusi juu ya sherehe hiyo ya kuzaliwa kwake katika kanisa la Mtakatifu George ambako alihubiri kwa muda mrefu.

Desmond Tutu hupenda kuzungukwa na watetezi wa haki

Wiki iliyopita, Wakfu wenye jina lake na mkewe Leah mwenye umri wa miaka 66, ulifanya mnada mtandaoni kwa kuuza vitu vya mshindi huyo wa tuzo ya Nobel, na kukusanya randi milioni 3 na nusu sawa na euro laki mbili. Wakfu huo pia utaandaa mkutano kwenye mtandao utakaohudhuriwa na Dalai Lama, Rais wa zamani Ireland Mary Robinson, mwanaharakati wa haki za binaadamu Graca Machel na Mpatanishi wa zamani wa Afrika Kusini Thuli Mandosela, aliependwa kutokana na ujasiri wake wa kukemea ufisadi wa serikali.

Tutu akiwa na Dalai LamaPicha: Kyodo/MAXPPP/picture alliance

Chaguo hili la washiriki linaonyesha maadili ya Desmond Tutu, ambae hupenda kuzunguukwa na watetezi wa haki katika kipindi ambacho wanasiasa wa nchi hiyo wanatajwa kutokana na nyumba zao za kifahari na utajiri wao binafsi. Mara ya mwisho Tutu kuonekana hadharani ilikuwa mwezi Mei mwaka huu wakati akipewa chanjo dhidi ya covid-19 akiwa kwenye kiti chenye magurudumu, alionekana mwenye tabasamu na alisalimia kwa mbali bila hata hivyo kuzungumza na waandishi wa habari.

Umri umesonga mbele na leo ni vigumu kukumbuka kuwa katika miaka ya 1960, Tutu aliesomea Theolojia (maswala ya dini) nchini Uingereza, alirejea nchini mwake na kukabiliana na fedheha sambamba na raia wenzake weusi. Binti yake Mpho Tutu Van Furth ambe walishirikiana kuandika vitabuviwili, alisimulia kuwa, siku moja wakati wa safari ya kifamilia, walisimama sehemu ili kununua barafu maana kulikuwa na joto kali.

Tutu alikuwa na ushawishi katika Kanisa la Kianglikana

Baba alipoingia ndani, mhudumu alimwambia kuwa hawahudumii ma "kaffirs" ndani ya duka, hivyo anatakiwa aagize akiwa nje na kupitia dirishani. Mpho alisema kuwa alimuona baba yake akitoka nje akiwa mwenye ghadabu na siku hiyo hawakupata kula barafu. Kaffir ni tusi baya zaidi na la kibaguzi nchini Afrika Kusini, yeyote anaelitumia kwa sasa, huweza kukabiliwa na mashtaka ya jinai.

Tutu na hayati Nelson MandelaPicha: Walter Dhladhla/dpa/picture alliance

Ushawishi wa Tutu ndani ya taasisi za Anglikana ulimsukuma katika mchakato wa kitaifa wa upatanishi na maridhiano na kusema kuwa nchi yake ni ya watu mchanganyiko, akiamini kwa dhati kuwa yaliyotokea nchini Afrika Kusini, yanaweza kuwa mfano wa kuigwa kwa mataifa mengine ulimwenguni katika kujifunza na kuelewa jinsi ya kumaliza mizozo ya kijamii.

Kiu yake ya msamaha wa kitaifa imekuwa ikikosolewa na kizazi kipya nchini humo ambapo watu weusi walijitolea mno katika mchakato huo wa makubaliano kuelekea demokrasia mwaka 1994, bila hata hivyo kuwawajibisha watekelezaji wa sera dhalimu ya Apartheid. Lakini kila mtu anakubali kuwa Desmond Tutu aliendelea kukemea vitendo vya uonevu na dhulma, alikosoa vikali kitendo cha Nelson Madela kuwapa mawaziri wake mishahara ya juu na pia ufisadi uliokithiri katika utawala wa rais Jacob Zuma.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW