Je, mkuu mpya Deutsche Bahn ataitoa kwenye mzozo wa kudumu?
23 Septemba 2025
Mara nyingi kuchelewa kwa saa kadhaa, kukosa treni za muunganiko, safari kufutwa, vituo vilivyochafuka, reli mbovu, mitambo iliyoharibika na ujenzi usiokoma. Ndani ya treni: huduma hafifu na vyoo visivyo safi. Kwa miaka mingi, Deutsche Bahn imezama katika mgogoro wa kudumu.
Sasa matarajio ni kwamba hali itabadilika – kwa usimamizi mpya, ratiba ya utekelezaji halisi, na mkazo katika jukumu la msingi: kuendesha treni zinazowasafirisha abiria kwa urahisi na kwa wakati.
Waziri wa Uchukuzi wa serikali ya Kansela Friedrich Merz, Patrick Schnieder, alimtambulisha Evelyn Palla Jumatatu mjini Berlin kama Mkurugenzi Mtendaji mpya na kuwasilisha pia mpango wa kuboresha reli.
Evelyn Palla: Mwanzo mpya reli ya Ujerumani
Evelyn Palla, mwenye umri wa miaka 51, mzaliwa wa Tyrol Kusini, Austria, alichukua nafasi ya Richard Lutz aliyeshindwa kufanikisha mageuzi. Katika mkutano wa waandishi wa habari Berlin, alisema: "Tunachukua mziki wa zama mpya – enzi ambayo tutazingatia tena kile kinachotufafanua: kuendesha treni, reli kama mshipa wa maisha wa taifa hili.”
Palla yupo kwenye bodi ya shirika la reli tangu 2019, na mwaka 2022 alihusishwa na usafiri wa kikanda. Amefanikiwa kuuboresha, na kwa mara ya kwanza uliandika faida. Mwaka jana hata alipata leseni ya kuendesha treni (Triebfahrzeugschein), ili kuelewa vyema kazi ya wafanyakazi wake na kile kinachounda biashara ya msingi ya kampuni.
Tatizo kuu: Kutofika kwa wakati
Waziri Schnieder alikosoa uongozi wa zamani akisema ahadi ya kufikia asilimia 75–80 ya treni kufika kwa wakati kufikia 2027 haiwezekani. Badala yake, ameweka lengo jipya: kufikia asilimia 70 ifikapo 2029.
Takwimu zinaunga mkono kauli yake: nusu ya kwanza ya mwaka huu treni za masafa marefu zilikuwa sahihi kwa asilimia 63.4 tu, mwezi Julai pekee zikishuka hadi asilimia 56.1.
Kwa maneno mengine: zaidi ya asilimia 40 ya treni hazikuwasili kwa wakati katika mwezi muhimu zaidi wa usafiri wa majira ya kiangazi. Kwa kulinganisha: Denmark na Uholanzi zina wastani wa asilimia 90, na Uswisi asilimia 99.
Schnieder alionya kwamba kushindwa kwa Deutsche Bahn kunaweza kudhoofisha imani ya wananchi kwa serikali: "Wengi wanahusisha matatizo ya reli na matatizo ya nchi. Hilo ni hatari kubwa.”
Mpango wa ukarabati mkubwa hadi 2036
Kufikia 2036, takriban njia 40 muhimu za reli zitasanifiwa upya. Mfano ni "Riedbahn” kati ya Frankfurt na Mannheim iliyofungwa kwa miezi mitano tu, ikikarabatiwa kwa gharama ya euro bilioni 1.3. Sasa, njia maarufu Berlin–Hamburg iko kwenye matengenezo hadi Aprili mwaka ujao kwa gharama ya euro bilioni 2.2.
Mwaka jana pekee, kilomita 2,000 za reli na vituo 2,000 vilirekebishwa, madaraja 150 na zaidi ya vituo 1,000 kusanifiwa. Gharama: euro bilioni 16.4. Reli itapata zaidi kutoka kwenye mfuko maalum wa euro bilioni 500 kwa ajili ya miundombinu na kidigitali.
Hata hivyo, changamoto zilibaki zikionekana papo hapo: Jumatatu hiyo hiyo, safari kati ya Hamburg na Berlin zilisitishwa kwa saa kadhaa kutokana na hitilafu ya umeme. Treni za ICE zilifutwa kabisa.
Kwa Evelyn Palla, mwanzo wake umejaa changamoto nyingi. Kama alivyoelezwa na wachambuzi: "Kuna kazi kubwa sana ya kufanya.”