DFB yapuuza malalamiko ya Bayern
16 Machi 2026
Shirikisho la Soka la Ujerumani (DFB) limepuuzilia mbali ukosoaji mkali uliotolewa na rais wa Bayern Munich, Uli Hoeness, kuhusu uamuzi wa refa katika sare ya 1-1 dhidi ya Bayer Leverkusen, ambapo Bayern ilipata kadi nyekundu mbili na mabao mawili yakakataliwa.
Wachezaji wa Bayern, Nicolas Jackson, alipewa kadi nyekundu ya moja kwa moja, na Luis Diaz alitolewa nje kwa kadi ya pili ya njano Jumamosi. Mabao ya Jonathan Tah na Harry Kane yalikataliwa kwa kuushika mpira. Leverkusen pia walinyimwa bao la Jonas Hofmann mwishoni kwa kuotea kwa tofauti ndogo sana.
Mwamuzi Christian Dingert alikiri baada ya mechi kuwa alikosea kumtoa Diaz kwa madai ya kujiangusha, huku Hoeness akiiambia gazeti la Bild kwamba "uamuzi mbaya zaidi wa waamuzi niliowahi kuona kwenye mechi ya Bundesliga."
"Hakuna Kashfa” – DFB
Msemaji wa kitengo cha waamuzi cha DFB, Alexander Feuerherdt, aliambia gazeti la AZ kwamba hawaungi mkono maoni ya Hoeness.
"Maamuzi muhimu ya mchezo yalikuwa sahihi au angalau yanaelezeka — isipokuwa kadi ya pili ya njano ambayo Dingert mwenyewe amekiri," Feuerherdt alisema. "Huenda maoni ya Hoeness yameathiriwa na ukweli kwamba maamuzi mengi yalikwenda kinyume na Bayern. Lakini hatuzungumzii makosa ya kashfa hapa."
Bayern walikasirishwa zaidi na kutolewa kwa Diaz, lakini pia na bao la Kane kukataliwa kwa madai ya kuushika mpira, wakati alipogongwa kwa karibu na kipa wa Leverkusen, Janis Blaswich, sekunde chache baada ya kuingia uwanjani.
Dingert alikiri makosa yake baada ya marudio kuonyesha kuwa kulikuwa na mguso kati ya Blaswich na Diaz. Alisema VAR haingeweza kuingilia kwa sababu sheria za sasa huruhusu ukaguzi kwa mabao na kadi nyekundu za moja kwa moja pekee.
Hata hivyo, Diaz bado atakosa mechi ijayo dhidi ya Union Berlin kwa sababu uamuzi wa uwanjani hauwezi kubatilishwa hata kama ulikuwa wa makosa.
Kocha wa Bayern, Vincent Kompany, alisema: "Sifurahii kwamba Lucho amefungiwa. Kulikuwa na mguso. Unaweza hata kujadili kama ni penalti, lakini si kadi ya njano."
Kuhusu bao la Kane kukataliwa, Tah alisema: "Huo sio kuushika mpira. Amegeuka tu.”
Kipa Sven Ulreich aliongeza: "Amepigwa kutoka umbali wa mita moja."
Mjumbe wa bodi ya Bayern, Max Eberl, alisema: "Ilionekana kama kila uamuzi wa 50-50 ulienda kinyume chetu.”
Kompany aliwasifu wachezaji wake kwa kupata pointi licha ya kuwa pungufu ya mchezaji mmoja kabla ya mapumziko, kusawazisha, na kisha kuhimili shinikizo wakiwa pungufu ya wachezaji wawili mwishoni.
"Ninajivunia sana nguvu ya kiakili ya wachezaji,” Kompany alisema.
Tah aliongeza: "Tulifanya kazi ya ajabu leo. Tulikataa kuruhusu hali ngumu kutuvunja moyo. Huo ndio uimara wa timu hii.”
Ulreich Arudi Uwanjani
Kipa Sven Ulreich, aliyekuwa anacheza mechi yake ya kwanza tangu Septemba 2024 na tangu kufiwa na mwanawe mwaka jana, alifanya kazi nzuri, akisaidia kulinda sare kwa kuokoa shuti muhimu dakika za mwisho.
"Ilipendeza kurudi uwanjani tena. Ilikuwa mechi maalum kwangu,” Ulreich alisema.
Hata hivyo, kulikuwa na habari mbaya Jumapili baada ya Bayern kuthibitisha kuwa Ulreich alipata jeraha la misuli litakalomuweka nje kwa muda. Klabu inatarajia Jonas Urbig atakuwa fit kufikia Jumatano kwa mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Atalanta, baada ya kupata mtikisiko wa ubongo kwenye mechi ya kwanza ambayo Bayern ilishinda 6-1.