1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dhahabu ya DRC yaporwa na majirani?

15 Juni 2020

Wataalamu wa UN wametoa ripoti inayobaini usafirishaji wa dhahabu ya DRC kwa njia za magendo kupitia Mashariki kuelekea nchi jirani za eneo hilo la maziwa makuu,huku Kampala kikitajwa kuwa kituo kikuu cha biashara hiyo

Samthandschuhe
Picha: Imago Images/blickwinkel

Ripoti ya Umoja wa Mataifa imeibaini  kwamba uchimbaji wa madini ya dhahabu katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo unaendelea kwa aina fulani kutoripotiwa inavyostahili wakati tani chungunzima za madini hayo ya tunu zikisafirishwa kwa magendo nje ya taifa hilo kwenye masoko ya dunia kupitia nchi jirani za taifa hilo kwa upande wa mashariki.

Nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zilizoko kwenye eneo la mpaka wake wa Mashariki kwa kipindi kirefu zinatumiwa kusafirisha madini ya dhahabu ya mabilioni ya dolla yaliyochimbwa kwa njia zisizo za kisasa na wale wanaoitwa wachimba migodi wadogo.  

Kutokana na kuwepo ugumu wa kufuatilia biashara ya madini hayo ya thamani  kumechochea vita vya kikanda,ufadhili wa makundi ya wapiganaji ya waasi pamoja na kusababisha vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya wafanyabiashara wanaojihusisha katika harakati za kufanikisha biashara ya usafirishaji madini hayo ya Congo.

Kundi la wataalamu wa Umoja wa Mataifa nchini humo limebaini kwenye ripoti yao ya mwaka kwamba katika mikoa ya Kivu Kaskazini,Kivu Kusini na Ituri imeripotiwa kwamba kiwango rasmi cha madini hayo kilichochimbwa na wachimbaji wadogo kilikuwa ni zaidi ya kilo 60 katika mwaka 2019 ingawa kiwango jumla cha dhahabu iliyosafirishwa ni zaidi ya kilo 73.

Kundi hilo la wataalamu limekadiria kwamba kiasi tani 1.1 ya dhababu ilisafirishwa kwa njia ya magendo kutoka mkoani Ituri katika mwaka 2019 pekee. Kiwango hicho cha dhahabu kingeiwezesha serikali kujipatia zaidi ya dola milioni 1.8 kupitia ushuru endapo ingesafirishwa kwa njia halali. Kwenye mikoa yote inakochimbwa dhahabu nchini humo inatajwa kwamba hasara iliyoshuhudiwa huenda ni kubwa zaidi.

Picha: Getty Images/AFP/L. Healing

Wachimbaji wadogo nchini Kongo wanachimba tani 15 hadi 22 za madini hayo kila mwaka kwa mujibu wa makadirio ya taasisi ya kijerumani ya masuala ya uchimbaji unaohusu ardhi na mali asili. Hata hivyo waziri anayehusika na madini wa Congo Willy Kitobo Samsoni, alipoulizwa na shirika la habari la Reuters kuhusu ripoti hiyo iliyotolewa,alisema hawezi kutowa jibu mara moja kuhusu kiwango cha madini kinachosafirishwa kwa njia za magendo kutoka mashariki mwa nchi hiyo.

Nchi jirani

Watalaamu wa Umoja wa Mataifa pia wamebaini kwamba Uganda na nchi nyingine jirani zinasafirisha kiwango kikubwa cha dhahabu kuliko kile kinachochimbwa na nchi hizo hali inayoashiria kwamba huenda zinahusika kwenye dhahabu inayosafirishwa kimagendo kutoka Kongo.

Zaidi ya asilimia 95 ya dhahabu  iliyosafirishwa mwaka 2019 kutoka Uganda ambayo ni kiasi zaidi ya tani 25 haikuwa dhahabu asili ya Uganda,kundi hilo la wataalamu limekadiria hayo kwa kuzingatia uzalishaji wa nchi hiyo wa mwaka 2018 na  takwimu za usafirishaji madini hayo ya mwaka 2019.

Picha: DW/S. Schlindwein

Takwimu za benki kuu mwezi Machi zilionesha kwamba kiwango cha dhahabu iliyosafirishwa kutoka Uganda iliongezeka zaidi ya mara mbili katika mwaka 2019 ikilinganishwa na miaka iliyopita. Waziri wa nishati wa Uganda naye hakujibu ombi la kumtaka atoe tamko kuhusu ripoti hii.

Lakini wasafirishaji magendo waliwaambia wataalamu kwamba Kampala ndio kituo kikuu cha biashara ya dhahabu kutoka mkoani Ituri. Dhahabu iliyosafirishwa kutoka Kivu Kusini ilipelekwa Burundi,Rwanda,Umoja wa Falme za kiarabu na Tanzania kwa mujibu wa ripoti hiyo.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri: Josephat Charo

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW