1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Muziki

Diamond Platnumz: Kutoka Tandale hadi kilele

12 Septemba 2026

Kutoka kuuza nguo Tandale hadi kutamba kwenye majukwaa ya kimataifa, Diamond Platnumz ameivusha Bongo Flava mipaka na kujenga himaya inayokuza wasanii wengine na kuifanya Tanzania isikike duniani.

Afrika Kusini 2022 | Diamond Platnumz katika kipindi cha uhalisia cha Netflix Young, Famous & African
Diamond Platnumz ameisaidia Bongo Flava kuvuka mipaka, kuvutia masoko ya kimataifa na kuwafungulia wasanii wengine wa Tanzania njia kupitia lebo yake ya WCB Wasafi.Picha: Netflix/Everett Collection/picture alliance

Diamond Platnumz ni miongoni mwa wasanii walioibadilisha Bongo Flava kutoka muziki wenye nguvu zaidi ndani ya Tanzania na Afrika Mashariki, hadi kuwa bidhaa inayosikilizwa na kutazamwa katika sehemu mbalimbali za dunia.

Jina lake halisi ni Naseeb Abdul Juma Issack. Alikulia Tandale, Dar es Salaam, katika mazingira ambayo hayakuwa na urahisi mkubwa wa maisha, lakini ndoto yake ya kuwa mwanamuziki ilianza kujengeka akiwa bado kijana.

Diamond alianza kuufuatilia muziki kwa umakini mwaka 2006. Ili kupata fedha za kurekodi, alifanya shughuli mbalimbali, ikiwemo kuuza nguo, na kutumia sehemu ya mapato yake kulipia muda wa studio.

Kupitia WCB Wasafi, Diamond amesaidia kukuza na kutambulisha wasanii kadhaa wa Tanzania.Picha: Frederick M. Brown/Getty Images

Hatua zake za kwanza hazikumletea mafanikio ya haraka. Alirekodi nyimbo ambazo hazikupata mwitikio alioutarajia, lakini aliendelea kutafuta watayarishaji, wasimamizi na nafasi ya kuifikisha sauti yake kwa mashabiki.

Mabadiliko makubwa yalikuja kupitia wimbo Kamwambie mwaka 2010. Wimbo huo ulimpatia umaarufu mkubwa na kushinda tuzo tatu katika Tanzania Music Awards, zikiwemo za msanii chipukizi, wimbo bora na wimbo bora wa R&B.

Kuzaliwa kwa nyota mpya

Mafanikio ya Kamwambie yalifuatiwa na nyimbo kama Mbagala, Nitampata Wapi, Nitarejea na Moyo Wangu. Nyimbo hizo zilimjengea Diamond sura ya msanii wa mapenzi mwenye sauti, uchezaji na uwezo mkubwa wa jukwaani.

Albamu yake ya kwanza, Kamwambie, ilitolewa mwaka 2010. Miaka miwili baadaye alitoa Lala Salama, ambayo iliendeleza ukuaji wake na kumweka miongoni mwa wasanii wakubwa zaidi Tanzania.

Lakini mafanikio yake hayakutokana na sauti pekee. Diamond alitambua mapema umuhimu wa picha, video zenye ubora, mavazi, uchezaji na namna ya kujitangaza. Hivyo, aliifanya kazi ya muziki kuwa kifurushi kamili cha burudani.

Wimbo Kamwambie wa mwaka 2010 ulimpatia Diamond Platnumz umaarufu mkubwa na kuwa mwanzo wa safari yake kuelekea kilele cha Bongo FlavaPicha: Hubert Boesl/dpa/picture alliance

Wimbo Number One na remix yake aliyomshirikisha Davido wa Nigeria vilikuwa hatua muhimu katika kupanua soko lake. Ushirikiano huo ulimsaidia kujulikana zaidi Afrika Magharibi na kuunganisha Bongo Flava na Afrobeats.

Mwaka 2014, Diamond alipata uteuzi wake wa kwanza wa tuzo za BET katika kipengele cha Best International Act: Africa. Uteuzi huo ulimweka katika kundi la wasanii waliokuwa wakiongoza muziki wa Afrika wakati huo. 

Kutoka msanii hadi kujenga taasisi

Kadiri umaarufu wake ulivyoongezeka, Diamond alipanua shughuli zake na kuanzisha lebo ya WCB Wasafi. Kupitia lebo hiyo, alitoka katika nafasi ya msanii pekee na kuwa mlezi, mwajiri na msimamizi wa vipaji vingine.

WCB Wasafi imewahi kuwalea au kuwasimamia wasanii kama Harmonize, Rayvanny, Mbosso, Lava Lava, Zuchu, Queen Darleen na D Voice. Baadhi yao walikuja kujenga majina makubwa ndani na nje ya Tanzania.

Mfumo huo ulionyesha kwamba mafanikio ya msanii mmoja yanaweza kutumiwa kujenga jukwaa la wengine. Pia uliimarisha ushindani wa kibiashara na kitaalamu katika tasnia ya muziki nchini Tanzania.

Mbali na muziki, Diamond Platnumz ni mjasiriamali aliyejenga biashara katika vyombo vya habari, usimamizi wa wasanii, kamari na bidhaa mbalimbali kupitia chapa ya Wasafi.Picha: Netflix/Everett Collection/picture alliance

Diamond aliendeleza upanuzi huo kupitia Wasafi Media na tamasha la Wasafi Festival. Hatua hizi zilisaidia kujenga mtandao unaounganisha muziki, redio, televisheni, matangazo na maonyesho ya moja kwa moja.

Mwaka 2017 alisaini mkataba na Universal Music Group. Albamu yake ya tatu, A Boy from Tandale, ilitolewa mwaka 2018 ikiwa na wasanii wa kimataifa kama Ne-Yo, Rick Ross, Morgan Heritage, Omarion, Tiwa Savage, Flavour na Davido.

Kuivusha Bongo Flava mipaka

Jina A Boy from Tandale lilibeba ujumbe kuhusu safari yake: kutoka mtaa wa kawaida jijini Dar es Salaam hadi kufanya kazi na baadhi ya majina makubwa katika muziki wa Afrika na Marekani.

Diamond aliendelea kutumia ushirikiano kama daraja la kuyafikia masoko mapya. Amefanya kazi na wasanii kama Koffi Olomide, Fally Ipupa, P-Square, Burna Boy, Alicia Keys, Innoss’B na Patoranking.

Kupitia nyimbo kama Nana, Marry You, Inama, Yope Remix, Jeje na Waah, alichanganya Bongo Flava na Afrobeats, rumba, ndombolo pamoja na mitindo mingine ya kisasa ya Afrika.

Mazunguzumzo ya Diamond Platnumz na DW

17:46

This browser does not support the video element.

Mwaka 2021, WCB Wasafi iliingia katika ushirikiano wa kimataifa na Warner Music Group. Hatua hiyo ilikuwa ishara ya namna biashara ya muziki wa Tanzania ilivyokuwa imeanza kuvutia kampuni kubwa duniani.

Diamond pia ametumia kwa nguvu majukwaa ya kidijitali. Mwaka 2025 alifikisha zaidi ya wafuatiliaji milioni 10 kwenye YouTube na kupokea Diamond Play Button, hatua iliyodhihirisha ukubwa wa hadhira yake nje ya mipaka ya Tanzania.

Mchango wake kwa Bongo Flava hauishii katika nyimbo na tuzo. Ameongeza thamani ya video za muziki, maonyesho, mikataba ya matangazo, usimamizi wa wasanii na matumizi ya mitandao katika kufikia mashabiki.

Katika safari ya miaka 30 ya Bongo Flava, Diamond Platnumz anawakilisha kipindi ambacho muziki huo ulivuka mipaka ya Tanzania na kuingia katika ushindani wa bara zima. Kutoka Tandale hadi majukwaa ya kimataifa, safari yake imeonyesha kwamba Bongo Flava inaweza kuwa muziki, biashara na chapa ya dunia.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW