1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

"Die Mannschaft" kupambana na Ireland

13 Oktoba 2014

Kipigo cha kwanza cha kihistoria, Poland kwa mara ya kwanza yaonja ushindi dhidi ya "Die Manschaft", Timu ya taifa ya Ujerumani.

EM-Qualifikation Polen - Deutschland 11.10.2014
Kikosi cha timu ya taifa ya Ujerumani Die ManschaftPicha: Reuters/Kacper Pempel

Muda hauko upande wa kocha Joachim Loew wa kutafakari kipigo mjini Warsaw dhidi ya Poland. Kocha wa Ujerumani anatakiwa kuchukua hatua za haraka kubadilisha mwelekeo wa majaaliwa ya kikosi hicho cha Die Mannschaft katika michezo ya kufuzu kucheza katika fainali za kombe la mataifa ya ulaya , Euro 2016 nchini Ufaransa.

Kuteleza tena kunaweza kukiweka kikosi hicho cha Joachim Loew katika hatari kubwa kesho Jumanne dhidi ya timu kutoka Ireland ambayo ina utamaduni wa kuipa shida Ujerumani uwanjani.

Wachezaji wa Poland wakifurahia bao laoPicha: Reuters/Kacper Pempel

Loew amesema kuwa tunapaswa kuzungumzia , vipi tunaweza kufunga mabao, kutokana na kupoteza nafasi kadhaa za kufunga mabao kama ilivyotokea katika mchezo na Poland siku ya Jumamosi , ambapo Ujerumani ilipata kipigo cha kwanza dhidi ya Poland cha mabao 2-0.

Ni kipigo cha kwanza katika michezo 33 ya kufuzu kucheza katika fainali - wakati kikosi cha kocha Loew hakikutumia fursa ilizopata.

Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Ujerumani Thomas Müller anaelezea hali ya mchezo ulivyokuwa, kwa kusema.

"Kimchezo nadhani hali ilikuwa nzuri tu. Hususan mwishoni mwa kipindi cha kwanza hatukupata idadi kubwa ya nafasi za kupata mabao na zile chache tulizozipata hatukuzitumia. Hapa ni lazima tujilaumu wenyewe."

Mats Hummels na wenzake wakitoka uwanjani wakiwa vichwa chiniPicha: picture-alliance/dpa/Thomas Eisenhuth

Dakika sita baada ya kuanza kipindi cha pili , mabingwa hao wa dunia waliinamisha vichwa. Milik wa Poland alipata bao alilolifunga kwa kichwa. Mlinda mlango Manuel Neuer hakuonekana katika hali nzuri.

Siku ya historia kwa Poland

Hii ni siku ambayo Wajerumani watapenda kuisahau haraka , lakini kwa Poland ni historia.

Mchezaji wa ulinzi wa Ujerumani Mats Hummels anasema.

"Nafikiri , tulikuwa tumeudhibiti mchezo, lakini magoli hayakupatikana kwa upande wetu. Wapinzani waliweza kufanya vizuri na hatimaye walipata ushindi wa mabao 2-0, bila shaka yoyote. Lakini hilo hutokea katika soka."

Kocha Joachim Löw wa Die ManschaftPicha: picture-alliance/dpa/T. Eisenhuth

meneja wa timu ya taifa ya Ujerumani Oliver Bierhoff hata hivyo , ameonya kwamba timu yake inapaswa kuonesha nini inachoweza kufanya haraka iwezekanavyo.

Tunakosa hivi sasa kuchukua hatua ya mwisho. Tumegharamika , lakini sitapenda kujiweka katika mtafaruku, amesema Bierhoff jioni ya jana mjini Gelsenkirchen, ambako utafanyika mchezo kati ya Ujerumani na Ireland hapo kesho.

Kikosi cha kocha Joachim Loew kinatambua kuwa kesho dhidi ya Ireland kinapaswa kucheza kwa kiwango cha juu na tunatarajia kupata jibu sahihi.

Rais wa UEFA Michel PlatiniPicha: Reuters/Denis Balibouse

"Mafanikio katika kupata magoli, hayana mahusiano na mbinyo uliopo. Hatuhitaji pia kufanya maajabu wakati wa matayarisho katika chumba cha kuvalia. Hii ni kitu ambacho kinaambatana na jinsi tunavyofikiri, ambapo nina maana kwamba kuna kitu kinakosekana katika umaliziaji."

"Die Mannschaft" uso kwa uso na Ireland

Ujerumani inakumbana na Ireland kesho Jumanne(14.10.2014) mjini Gelsenkirschen , wakati kikosi cha Martin O'Neill kikitafuta kwa mara ya kwanza kupata ushindi dhidi ya mabingwa hao wa dunia katika muda wa miaka 20.

Ireland ilipata ushindi dhidi ya Ujerumani wa mabao 2-0 Mei mwaka 1994 wakati Tony Cascarino na Gary Kelly walipoipatia Ireland mabao mjini Hannover katika mchezo wa kirafiki na kikosi hicho kinamatumaini ya kuwafumania wenyeji wao wakiwa bado hawajaamka baada ya kipigo dhidi ya Poland.

Kwa kulinganisha Ireland inajiamini baada ya kuirarua Gilbralter kwa mabao 7-0 mjini Dublin na kuchupa hadi nafasi ya pili katika kundi D nyuma ya viongozi wa kundi hilo Poland.

Wakati huo huo Scotland inapambana na viongozi wa kundi hilo Poland mjini Warsaw kesho katika mchezo wa kundi D.

Michezo mingine ya Euro 2016 , ni pamoja na Iceland itapambana na Uholanzi na Malta itakwaana na Italia, wakati Kazakhstan ina miadi na Jamhuri ya Czech.

Michel Platini katika kurunzi

Wakati rais wa shirikisho la kandanda barani Ulaya Michel Platini alipobadilisha mfumo wa fainali za kombe la mataifa ya Ulaya , kutoka ule mgumu wa timu 16 katika fainali za mwaka 2012 na kuwa kila mmoja anakaribishwa kwa kuzifanya timu hizo kufikia 24 katika michuano ya fainali mwaka 2016, haikushangaza kwamba alikumbana na ukosoaji mkubwa.

Alionekana kuwa amechafua mfumo ambao ulikuwa katika hali nzuri kabisa ambao haukutakiwa kuchafuliwa. Kwa sasa hata kwa timu bora kabisa kutoka bara la Ulaya , kufuzu kucheza katika fainali si jambo la kuumiza kichwa, na haki yao.

Nadharia ya sasa ni kwamba , timu mbili ama hata tatu kutoka katika kundi moja zina uhakika wa kuingia katika fainali . Vigogo vya soka barani Ulaya vinaweza kucheza bila kujali sana kufungwa na hatimaye zitakuwa salama kufikia fainali.

Na ndio huenda sababu ya timu nyingi vigogo katika bara hilo , zinaweza kukubali kwa kiasi kikubwa kucheza bila ya makini na kufungwa , kwamba wanaweza kujirekebisha baadaye. Ureno imefungwa na Albania , Ujerumani na Poland , Uhispania nayo dhidi ya Slovakia.

Kocha wa Nigeria Stephen KeshiPicha: Pius Utomi Ekpei/AFP/Getty Images

Wadadisi wa masuala ya soka wanahisi kuna sababu nyuma ya vipigo hivi.

Nigeria bado inasuasua

Lakini si katika bara la Ulaya tu mshangao ulipotokea, lakini hata katika bara la Afrika ambako mbinyo unaongezeka dhidi ya kocha wa Nigeria Stephen Keshi, kutokana na jinsi anavyoiendesha timu hiyo ya taifa na kwamba mabingwa hao wa Afrika wako katika hatari ya kushindwa kufikia fainali za mwaka ujao za kombe la mataifa ya Afrika nchini Morocco.

Tai hao wa kijani walikubali kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Sudan na kwa sasa iko mkiani mwa kundi lao la A, ikiwa na pointi moja tu kibindoni baada ya michezo mitatu. Nigeria ikumbana tena na Sudan katika mchezo utakaofanyika siku ya Jumatano mjini abuja.

Wakati Taifa Stars ya Tanzania imeiadhibu Benin kwa kuichapa mabao 4-1 mjini Dar Es Salaam , kocha wa timu hiyo Mart Nooij amesema mchezo huo ni kujitayarisha na kombe la mataifa ya Afrika mashariki na kati la Challenge litakalofanyika baadaye mwaka huu.

Kenya nayo inaingia uwanjani leo kupambana na Morocco katika mchezo wa kirafiki na itakuwa bila ya mshambuliaji wake Dennis Oliech.

Oscar Pistorius akiingia mahakamaniPicha: Reuters/Mike Hutchings

Brazil inakipiga leo nchini Singapore dhidi ya Japan baada ya kuwaangusha mahasimu wao wa Amerika ya kusini Argentina kwa mabao 2-0 siku ya Jumamosi.

Pistorius arejea mahakamani

Mkimbiaji nyota mlemavu Oscar Pistorius amerejea mahakamani leo , wakati kikosi chake cha mawakili kikitarajia kudai , mwanariadha huyo apewe adhabu ambayo si ya kifungo baada ya kumpata na hatia ya mauaji sawa na kuuwa bila kukusudia.

Mkimbiaji huyo ambaye anakimbia kwa miguu ya bandia alipatikana na hatia ya uzembe unaostahili adhabu , lakini hakupatikana na hatia ya kuuwa kwa kukusudia katika kifo cha mpenzi wake Reeva Steenkamp, hukumu ambayo iliwashangaza watu nchini humo na kuchochea ukosoaji wa mfumo wa sheria nchini Afrika kusini.

Chicago Marathon

Nae Eliud Kipchoge na Rita Jeptoo kutoka Kenya wameshinda mbio za Marathon za Chicago jana Jumapili , wakikamilisha ushindi mara nne wa wanariadha kutoka Kenya katika mbio hizo. Kipchoge , ambaye ni bingwa mara mbili wa Olimpiki wa mbio za mita 5,000 akishindana kwa mara ya nne katika mbio hizo za maili 26.2, alishinda kwa saa mbili , dakika nne na sekunde 11 akimshinda Mkenya mwenzake Sammy Kitwara kwa sekunde 17.

Rita Jeptoo mshindi wa Chicago Marathon kwa wanawakePicha: AFP/Getty Images

Dickson Chumba alikuwa wa tatu. Jeptoo alitetea ubingwa wake kwa kukimbia kwa saa mbili. dakika 24 na sekunde 35 akifuatiwa na Muethiopia Mare Dibaba.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre / dpa

Mhariri: Yusuf Saumu