1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dimba la Champions League.

15 Aprili 2009

Duru ya pili ya robo fainali ya kombe la klabu bingwa barani Ulaya, Champions League, inafanyika leo, pale Porto watakapowaalika mabingwa watetezi Manchester United.

Mechi ya Champions League kati ya Liverpool na Chelsea.Picha: AP

Arsenal itakuwa nyumbani, Emirates kuchuana na waspaniola Villareal. Iwapo mambo yatakuwa kama yalivyokuwa katika mechi za jana, wapenzi wa soka wasubiri msisimko. Chelsea jana ilijikatia tiketi ya nusu fainali, lakini baada ya kutolewa jasho na Liverpool. Mabingwa wa Ujerumani Bayern Munich walihitaji miujiza dhidi ya Barcelona.


Fabio Aurelio wa Liverpool, akisherehekea bao lake dhidi ya Chelsea, Stamford Bridge.Picha: AP

Manchester United, walio na shabaha ya kujipatia vikombe vitano msimu huu watakuwa Porto kujaribu kutimiza ndoto yao. Lakini Porto waliowaondoa Man U katika dimba hili mwaka wa 2004, watajaribu kuwazima na mapema hasa kwa kuwa walifanikiwa kutoka sare ya mabao mawili kwa mawili na Man U nyumbani Old Trafford wiki jana. Kibarua sasa itakuwa ni kwa vijana kwa Alex Ferguson....


Mechi ingine katika duru hii ya pili ni kati ya Arsena na Villareal wa uhsipania. Vijana wa Arsene Wenger watatumia kurejea kwa kapteini wao Cesc Fabregas na kuwa jogoo lao Emmanuel Adebayor ameshika makali katika safu ya ushambulizi kuwazima Villareeal kufika katika nusu fainali yao ya kwanza ya Champions League. Timu hizi mbili zilitoka sare ya 1-1, nchini Uhispania wiki jana.


Lakini mambo yalikuwa jana, uwanjani Stamford Bridge. Chelsea ilidhani imemaliza kazi karika raudni ya kwanza walipoicharaza Liverpool nyumbani mabao 3-1. Lakini ndio ilikuwa mwanzo mkoko unaalika maua.


Mabingwa watetezi wa kombe la klabu bingwa barani Ulaya, Manchester United watakutana usiku na Porto.Picha: AP

Bila ya nahodha wao Steven Gerrard, na kumbukumbu ya mkasa wa Hilsboruogh, ukiwa fikrani mwao, Liverpool walichukua usukani dakika 19 tu katika kipindi cha kwanza Fabio Aurelio akafungua awamu ya mabao ya Liverpool. Xavi Alonso akafunga bao la pili, alipopachika mkwaju wa penalti, baada ya kufanyikwa madhambi na Mserbia Ivanovic. Ivanovic alikuwa nyota ya Chelsea, alipowafungia mabao mawili huko Anfield wiki jana. Wakielekea katika kipindi cha mapumziko. Liverpool ilikuwa kileleni mabao 2-0.


Kocha wa Chelsea Mdachi Guus Hiddink hakuridhishwa na uchezaji wa wachezaji wake-ujumbe aliofikisha wakati wa mapumziko. Na waliporejea Chelsea hawakupoteza wakati katika dakika sita, wakafunga mabao mawili. Muivory Coast Didier Drogba na Mbrazil Alex wakarejesha matumaini kwa vijana wa Blues.


Pale Frank Lampard alipofunga bao la tatu la Chelsea, dau la Liverpool likawa linayumbayumba. Hata hivyo, Lukas na Dirk Kuyt wakafungia Liverpool bao la tatu na la nne mtawalia. Lakini Lampard akarejea tena na bao la nne la Chelsea.


Mabao manane Stamford Bridge, ikawa mwisho wa safari ya Liverpool, katika dimba la Champions League. Chelsea ikajikatia tiketi ya nusu fainalia kwa mabao 7-5.


Nchini Ujerumani Bayern Munich mabingwa wa Bundesliga walihitaji miujiza kuwazima, wacatalans, Barcelona- baada ya kuonyeshwa kivumbi Nou Camp wiki jana walipocharazwa mabao 4-0. Mfaransa Frank Ribery akafunga angalau bao la kufuta machozi. Barcelona haikulala ikajibu kupitia Seydou Keita.Ikawa 1-1,lakini tayari Barcelona, walikuwa wamemaliza kazi nyumbani wiki jana.


Sasa Barcelona watakutana na Chelsea katika nusu fainali.


Mwandishi Munira Muhammad/ AFP

Mhariri: Mohammed Abdulrahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW