Kwa nini Trump anaishinikiza India kununua mafuta yake?
4 Februari 2026
Rais Donald Trump na waziri mkuu wa India Narendra Modi walitangaza mnamo siku ya Jumatatu kuwa nchi hizo mbili zimefikia mkataba wa kibiashara kufuatia majadiliano makali na ya muda mrefu ingawa maelezo ya kina bado hayakutolewa. Chini ya mkataba huo, Marekani itapunguza ushuru wake wa bidhaa za India kwa asilimia 18 kutoka 25 huku Modi akijitolea kununua bidhaa zenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 500 kutoka Marekani-zikijumuisha bidhaa za nishati, teknolojia, kilimo na bidhaa nyinginezo.
India ambayo ni mwagizaji wa tatu wa mafuta duniani, pia ilikubali kusitisha hatua yake ya kununua mafuta ya Urusi na kuahidi manunuzi zaidi ya mafuta kutoka Marekani pamoja na uwezekano wa kununua mafuta kutoka Venezuela. Hata hivyo, wajuzi wanasema mkataba huo unaonekana kutimiza malengo mawili ya Ikulu ya White House.
Trump na ndoto za kuuhusisha uchumi wa Venezuela
Trump anadai kuwa anataka kuifufua sekta ya mafuta ya Venezuela baada ya Washington kuchukua udhibiti kamili wa sekta hiyo iliyokuwa ikidorora, kufuatia kukamatwa kwa Rais Nicolás Maduro na Marekani mwezi uliopita. Pili, Trump analenga kuongeza shinikizo kwa Moscow kuondoa uuzaji wa bidhaa ya mafuta ghafi ya Urusi kutoka Asia mojawapo ya masoko yake makubwa ya mwisho baada ya vikwazo vya Nchi za Magharibi kuwekwa kwenye mauzo yake ya nje yanayosaidia kufadhili vita vya Urusi nchini Ukraine.
Hatua za Marekani na serikali ya mpito ya Venezuela
Marekani na serikali ya mpito ya Venezuela wamechukua hatua kadhaa za kufufua sekta ya mafuta iliyodorora. Hatua hizo zinajumuisha kukubali kuuza hadi mapipa milioni 50 ya mafuta ghafi ya Venezuela — mengi yakienda kwa wasafishaji wa Marekani; kubadili sheria za mafuta na gesi za nchi hiyo ili kuvutia uwekezaji wa kigeni; na kulegeza baadhi ya vikwazo dhidi ya mauzo ya mafuta ya Caracas.
Asia huenda mwanzoni ikaonekana kama mshirika katika juhudi hizi. China ilinunua zaidi ya nusu ya mauzo ya mafuta ghafi ya Venezuela mwaka uliopita, huku wasafishaji huru wakichukua mafuta yaliyopunguzwa bei sana kutokana na vikwazo vya Marekani. India, ambayo hapo awali ilikuwa mnunuzi mkubwa, ilisitisha ununuzi wake tu baada ya Trump kuongeza ushuru wa 25 mwezi Machi kwa nchi zinazonunua mafuta ya Venezuela.
Mafuta ghafi ya Venezuela huenda yasibadili upepo
Lakini licha ya juhudi za karibuni za Trump, mafuta ghafi ya Venezuela hayatarajiwi kuwa na nafasi kubwa katika mfumo wa usafishaji mafuta wa Asia hivi karibuni hususan nchini India.
India, mnunuzi mkubwa zaidi wa mafuta ya Urusi yaliyopunguzwa bei baada ya uvamizi wa Ukraine mwaka 2022, ilipunguza ununuzi wake baada ya Trump mwezi Agosti kuongeza ushuru wa bidhaa zinazoingia kutoka India hadi 50 ili kuishinikiza New Delhi kupunguza ununuzi wake wa mafuta ya Urusi. Licha ya makubaliano ya kibiashara, usafirishaji wa mafuta ya Urusi kwenda India hautarajiwi kukoma.