1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dirk Niebel aitembelea Somalia

2 Aprili 2012

Waziri wa misaada ya maendeleo wa Ujerumani, Dirk Niebel, amefanya ziara ya ghafla nchini Somalia. Waziri huyo alifanya mazungumzo na serikali ya mpito ya Somalia pamoja na wawakilishi wa taasisi za kimataifa.

Dirk Niebel akiwa Somalia Mogadischu
Dirk Niebel akiwa Somalia MogadischuPicha: picture-alliance/dpa

Dirk Niebel amekuwa waziri wa kwanza wa Ujerumani kuitembelea Somalia katika kipindi cha miaka 19. Mwansaiasa huyo wa chama cha kiliberali cha FDP aliwasili Mogadishu, mji mkuu wa Somalia, Jumamosi baada ya hatua za muhimu za kuisalama kuchukuliwa. Mbali na kufanya mazungumzo na serikali ya Somalia, Niebel alikutana pia na wawakilishi wa Umoja wa Matafa, wanajeshi wa AMISOM na pia mashirika yasiyo ya kiserikali kama vile shirika la kusaidia watoto mayatima liitwalo SOS Children's Villages.

Mwaka 1977 utawala wa Somalia ulikiruhusu kikosi maalum cha polisi wa Ujerumani, kijulikanacho kama GSG 9, kuingia Mogadishu na kuikoa ndege ya shirika la Kijerumani la Lufthansa kutoka katika mikono ya magaidi wa Kipalestina. Niebel alipokuwa Somalia alisema: "Miaka 35 baada ya Somalia kuisaidia Ujerumani kupambana na ugaidi, umefika wakati wa Ujerumani kuonyesha kwamba inaisaidia Somalia katika kupambana na ugaidi na katika kujenga upya taifa huru."

Kituo cha SOS Children's Village cha MogadishuPicha: SOS-Kinderdörfer-Archiv

Hali tete ya kiusalama

Mwezi Februari mwaka huu, jumuiya ya kimataifa ilifikia uamuzi wa kurejesha upya hali ya usalama nchini Somalia. Kwa sasa, serikali ya mpito inalitawala eneo la mji mkuu, Mogadishu. Hivyo Dirk Niebel pamoja na ujumbe wake waliweza kuthubutu kutua katika mji huo. Ndege ya jeshi la Ujerumani iliyombeba waziri huyo ilileta pia vifaa vya msaada. Niebel vile vile alitoa msaada wa kifedha wa Euro millioni 6.3. Sehemu ya fedha hiyo itatumika kwa ajili ya kujenga upya kituo cha kulelea watoto cha SOS Children's Village, kilichobomolewa mwaka jana katika mapigano baina ya majeshi ya serikali ya Somalia na waasi wa kundi la kiislamu lenye itikadi kali la Al-Shabab.

Bado ni vigumu sana kupeleka msaada Somalia. Kundi la Al-Shabab limeyaambia mashirika yanayotoa misaada kwamba hayatakiwi kuwepo katika maeneo yanayotawaliwa na waasi hao. "Kwa sababu hiyo hakuna uwezekano wa kupeleka misaada inayohitajika," anaeleza Axel Rottländer wa shirika la kutoa misaada la CARE. "Yapo mashirika mengi, likiwemo shirika la CARE, ambayo hayawezi kufanya kazi huko kwa sababu za kiusalama kwani hata wafanyakazi wanaweza kutekwa nyara." Mwezi Desemba mwaka jana, wafanyakazi wawili wa shirika la Madaktari wasio na Mipaka waliuliwa mjini Mogadishu.

Wapiganaji wa kundi la Al-ShabaabPicha: AP

Ukame watishia maeneo ya kaskazini

Hata hivyo yapo pia maeneo yenye amani nchini Somalia, kama vile mikoa ya Puntland na Somaliland iliyoko kaskazini mwa nchi hiyo. Hata hivyo, mikoa hiyo haitambuliwi kimataifa. Shirika la CARE linajenga au wakati mwingine kukarabati visima katika maeneo hayo. Hilo ni jambo la muhimu kwani kuna hatari ya kutokea ukame. Inawezekana mvua zinazotarajiwa kunyesha mwezi Mei na Juni huu zikakosekana mwaka huu.

Axel Rottländer anaeleza kwamba jambo hilo lingekuwa na athari kubwa sana. Watu wengi wangekosa chakukla kwa sababu ya kutokuwepo kwa visima na maji. Hata mifugo ingekufa kwa njaa na kiu. "Watu hawatakuwa na namna. Watalazimika kuyaacha makazi yao na kukimbilia Mogadishu au Dadaab," anaeleza Rottländer. "Dadaab ni kambi ya wakimbizi kubwa kuliko zote Kenya. Wakati huu patakuwepo na wakimbizi wapatao 400,000 kutoka Somalia."

Kambi ya wakimbizi Dadaab, KenyaPicha: picture alliance/dpa

Lakini hata mji wa Mogadishu unakimbiliwa na mamia kwa maelfu ya watu wanaojaribu kuepuka janga la njaa. Waziri Dirk Niebel ameeleza kwamba wakimbizi hao lazima wapewe misaada pindi litakapotokea janga jingine la ukame. Lakini tayari sasa huduma ya maji si ya uhakika na vile vile yapo maeneo machache tu ambapo kuna huduma ya kuondoa maji taka. Niebel aliongeza kwamba hata huduma ya umeme na ya afya ambayo Ujerumani inasaidia kuileta, haitaweza kuondoa kabisa matatizo yaliyopo Somalia. Alisisitiza pia kwamba matatizo yatakwisha tu iwapo Somalia itakuwa na amani na uongozi bora. Mwishoni waziri huyo aliahidi kuitembelea tena Somalia baada ya miaka miwili.

Mwandishi: Christoph Käppeler

Tafsiri: Elizabeth Shoo

Mhariri: Saumu Yusuf