Djokovic arudishwa kwao Serbia
17 Januari 2022Ndege iliyombeba nyota huyo ilitua katika uwanja wa ndege wa Belgrade Jumatatu na kutilia kikomo taarifa ambayo imegonga vichwa vya habari vya michezo, siasa za virusi vya corona Australia na kuuzidisha mjadala kuhusiana na chanjo ya virusi hivyo.
Djokovic alikuwa anatarajiwa kulakiwa na maelfu ya mashabiki ila ni wachache tu walioonekana katika uwanja wa ndege wakiwa na bendera za Serbia.
Mchezaji wa Uhispania Rafael Nadal amesema kwa upande mwengine Djokovic anastahili kulaumiwa pia kwa yaliyomkuta.
"Kwa kweli namtakia kila heri, hali haijawa nzuri. Yeye pia anastahili kupokea lawama katika hali hii jinsi ilivyokwenda na kivyangu ningependa sana kumuona akishiriki mashindano haya ya Australian Open," alisema Nadal.
Huku hayo yakiarifiwa kuna kiwingu kuhusiana na mustakabali wa mchezaji huyo katika mchezo wa Tennis iwapo ataendelea na msimamo wake wa kutopokea chanjo.
Maafisa nchini Ufaransa wamesema sheria mpya nchini humo inayohitaji kila mmoja anayeingia katika uwanja wa michezo awe amechomwa chanjo ya virusi vya corona, haitombagua yeyote yule. Mashindano ya French open nchini Ufaransa yatakuwa yanafnyika mwezi mei, na mengi yanaweza kubadilika kutoka sasa hadi wakati huo ila iwapo atashikilia msimamo wake basi huenda asishiriki pia mashindano hayo makubwa ya Tennis nchini Ufaransa.