Djotodia avunja bunge la Jamhuri ya Afrika ya Kati
26 Machi 2013Michel Djotodia, mwanadiplomasia wa zamani aliyegeuka na kuwa muasi, ametangaza kuifuta katiba pamoja na kulivunja bunge na serikali. Kiongozi huyo amesema ataiongoza nchi hiyo kwa kutumia amri hadi uchaguzi utakapofanyika miaka mitatu ijayo. Akizungumza katika mahojiano na Radio France International, kiongozi huyo wa waasi amesema uchaguzi wa kitaifa utafanyika mwaka 2016. Hata hivo, amesema kuwa atauendeleza mkataba wa kugawana madaraka uliosainiwa baina ya waasi wa Seleka na rais wa nchi hiyo, Francois Bozize.
Djotodia amechukua madaraka ya nchi hiyo, baada ya kundi waasi wa Seleka kuuteka mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Bangui katika mapinduzi yaliyosababisha mauaji ya wanajeshi 13 wa Afrika Kusini. Hatua hiyo ilisababisha Rais Bozize kukimbilia nchi jirani ya Cameroon. Nchi hiyo imethibitisha kuwa Rais Bozize aliwasili nchini humo, lakini imesema haitampa kiongozi huyo ukimbizi wa kudumu, bali amepewa hifadhi ya muda.
AU yaisimamisha Jamhuri ya Afrika ya Kati uanachama
Mapema jana Jumatatu, Umoja wa Afrika uliisimamisha nchi hiyo uanachama, huku Umoja wa Ulaya ukilaani vikali mapinduzi hayo. Mapinduzi hayo yamelaaniwa pia na Umoja wa Mataifa, ambapo Katibu Mkuu wa umoja huo, Ban Ki-Moon amelaani kile alichokiita kuchukua madaraka kwa njia isiyo ya kikatiba na kutoa amri ya kurejeshwa kwa utawala wa katiba haraka iwezekanavyo. Nalo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekutana jana baada ya Ufaransa kuitisha kikako cha dharura kuzungumzia mzozo huo wa Jamhuri ya Afrika ya Kati. Huku ikitishia kuchukua hatua zaidi, baraza hilo halijatangaza kitisho cha kuweka vikwazo.
Taarifa zinaeleza kuwa Djotodia ambaye amejitangaza kuwa rais, ameomba msaada wa wanajeshi wa kulinda amani katika ukanda huo, ili kusaidia kurejesha utulivu baada ya wapiganaji wake kuendelea na uporaji kwa siku ya pili katika mji mkuu wa Bangui. Kiongozi huyo ametangaza amri ya kutotembea wakati wa usiku kuanzia saa moja kamili jioni hadi saa 12 kamili asubuhi.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa India, Manmohan Singh ameelezea masikitiko yake kutokana na mauaji ya wanajeshi wawili wa India waliouawa na wanajeshi wa Ufaransa, wakati wa mapinduzi hayo. Katika taarifa yake, Singh amesema wanajeshi hao walikuwa wanaulinda uwanja mkuu wa ndege wa Jamhuri ya Afrika ya Kati. Sigh amesema amepokea barua kutoka kwa Rais Francois Hollande akielezea masikitiko yake kutokana na vifo hivyo vilivyotokea kwenye mazingira ya kutatanisha. Kiongozi huyo wa India, ametoa maagizo ya kuhakikisha usalama unakuwepo dhidi ya kiasi raia 100 wa India walioko nchini humo.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,RTRE
Mhariri: Iddi Ssessanga