Dola bilioni 50 zahitajika kuhifadhi mazingira
30 Novemba 2009Mabadiliko ya hali ya hewa yanaziathiri sekta zote ikiwemo ya uchumi.Kwa mujibu wa mkurugenzi wa zamani wa Benki ya Dunia endapo hatua madhubuti hazitochukuliwa kupambana na hali hii kiasi cha asilimia 5 hadi 20 cha pato la ulimwengu huenda kikahitajika kuigharamia kazi hiyo.
Kwa mujibu wa ripoti ya Stern iliyochapishwa mwaka 2006 ulimwengu utalazimika kutumia asilimia moja ya pato lote endapo mataifa yataamua kupambana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa haraka iwezekanavyo.Kwa upande mwengine kutochukua hatua zozote huenda kuzigharimu hatua hizo kiasi cha kati ya asilimia 5 hadi 20 kila mwaka ili kupambana na athari za muda mrefu. Athari hizo huenda zikalifanya eneo la kusini mwa Bara la Ulaya kuwa kame au kugeuka kuwa majangwa kama vile Sahara na mengine kama Bangladesh kukumbwa na mafuriko.
Theluji ya milima ya Himalaya inapoyeyuka itaisababisha mito kujaa na kufurika baada ya maji kukipita kina chake jambo litakalowaathiri wengi na mafuriko.Hilo litasababisha ongezeko la umasikini,idadi ya wahamiaji vilevile ghasia.Kulingana na Lord Nicholas Stern aliyeiandaa ripoti hiyo ya mwaka 2006 hali hii itashuhudiwa kote ulimwenguni endapo hatua za dharura hazitochukuliwa,''Sharti tuuonyeshe ukubwa wa athari hizo na tusiishie hapo tu.Lazima tukifafanue kinachoweza kufanyika na hicho ndicho kinachotuchagiza,''alifafanua.
Kulingana na Nicholas Stern hatua nyingi zinaweza kuchukuliwa ili kupambana na athari hizo kwa madhumuni ya kuwa na ulimwengu ulio msafi na mahali salama.Mchumi huyo aliyepia mtaalam wa masuala ya hali ya hewa anayeusambaza ujumbe huo kote ulimwenguni ametuzwa hivi karibuni shahada ya udaktari ya heshima.Alituzwa shahada hiyo na Chuo Kikuu cha Ufundi cha Berlin.Nicolas Stern alilitilia mkazo suala la kuwa na mabadiliko katika sekta ya nishati na viwanda. Kwa sasa kiwango cha gesi za viwanda kimefikia takriban tani bilioni 50.Sharti kiwango hicho kipungue hadi tani bilioni 30 kwa mwaka ifikapo mwaka 2030 na kiwango hicho kishuke zaidi hadi tani bilioni 20 kwa mwaka ifikapo mwaka 2050.
Mageuzi hayo katika sekta ya viwanda sharti yaibadili teknolojia ya sasa inayotoa viwango vikubwa vya gesi zinazoyaathiri mazingira.Teknolojia hizo mpya zinapaswa kuwa na manufaa katika mazingira.Hata hivyo changamoto zipo,''Hilo linatuonyesha kibarua kikubwa kilichopo.Lazima tuvumbue mbinu za kuzalisha nishati ambazo hazitoi gesi za caboni ifikapo mwaka 2050…vilevile njia za usafiri na mbinu za kilimo.Sharti tupunguze ukataji wa miti,''alisisitiza.
Lengo hasa la kuzichukua hatua hizo ni kila mtu kote ulimwenguni apunguze kiwango cha gesi za viwanda katika mazingira kwa tani mbili kila mwaka.Ripoti hiyo iliyochapishwa mwaka 2006 kwa niaba ya serikali ya Uingereza ilijaribu kuzikadiria gharama za kupambana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa.Hasa ni kiasi kipi cha fedha kinachohitajika?''Kwa mtazamo wangu kiasi cha dola bilioni 50 kwa mwaka zinahitajika kupambana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa ifikapo mwaka 2015 ili tuweze kuvitimiza vigezo hivyo.Kiasi cha hicho ni sawa na asilimia 0.1 ya pato la ndani la mataifa tajiri.'' Hata hivyo suala nyeti hapa si la pesa tu kuna uwekezaji.Hii ni kwasababu mbinu mpya zitakazovumbuliwa sharti ziende sambamba na ukuaji wa uchumi na pato kwa jumla ili ulimwengu uweze kuwa salama na mahala safi pa kuishi.
Mwandishi:Thelma Mwadzaya/ZPR-Bettina Marx
Mhariri:Abdul-Rahman