"Dola la Kiislamu" ladhibiti nusu ya Syria
21 Mei 2015Mafanikio hayo mawili ya IS yameongeza shinikizo siyo tu kwa serikali za Syria na Iraq, lakini pia kuutilia shaka mkakati wa Marekani wa kuyategemea kwa kiasi kikubwa mashambulizi ya kutokea angani ili kulishinda Dola la Kiislamu. Kundi la IS limesema katika taarifa kuwa limechukua udhibiti kamili wa Palmyra, ikiwa ni pamoja na kambi zake za kijeshi, kuashiria mara ya kwanza limeukamata mji kutoka kwa jeshi la Syria na vikosi vinavyoongozwa na Marekani.
Shirika linalofuatilia haki za binaadamu la Syria limesema IS sasa inadhibiti zaidi ya nusu ya taifa la Syria kufuatia zaidi ya miaka minne ya mgogoro ambao ulitokana na vuguvugu la kumpinga Rais Bashar al-Assad. Shirika la Umoja wa Mataifa la masuala ya Utamaduni – UNESCO limeutaja mji wa Palmyra kuwa makutano ya kihistoria kati ya Himaya ya Kirumi, India, China na Uajemi ya kale. Wanajeshi 100 wa serikali ya Syria waliuawa katika mapambano ya eneo hilo.
Chombo cha habari cha serikali ya Syria kimesema wanajeshi wanaoiunga mkono serikali waliwahamisha raia kutoka eneo hilo kabla ya wao kuondoka. Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini ameelezea wasiwasi kuwa maelfu ya watu mjini Palmyra wanakabiliwa na kitisho pamoja na maeneo ya turathi za kale. Amesema uharibifu huo ni sawa na uhalifu wa kivita.
Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Urusi Sergei Lavrov amesema Urusi iko tayari kuipa Iraq silaha ili kuisaidia kupambana na wapiganaji wa IS. Lavrov aliyasema hayo kabla ya mazungumzo kati ya Rais wa Urusi Vladmir Putin na Waziri Mkuu wa Iraq Haider al Abadi mjini Moscow. Kuanguka mji wa Palmyra kumekuja siku tano tu baada ya IS kuikamata Ramadi, mji mkuu wa mkoa mkubwa kabisa wa Iraq, Anbar.
Kukamatwa mji wa Ramadi ni pigo kubwa sana kwa serikali ya Iraq. Marekani inapanga kupeleka Iraq silaha 1,000 za kuharibu vifaru na magari ya kijeshi mwezi Juni ili kupambana na mabomu ya kujitoa mhanga kama yale yaliyolisaidia kundi hilo la itikadi kali kuukamata mji wa Ramadi. Serikali ya Iraq imewaamuru wapiganaji wa Kishia, wengi wao wakiwa na mahusiano na Iran, kujiunga katika vita vya kuikomboa Ramadi na kuongeza hofu ya kuzuka upya machafuko ya kimadhehebu nchini humo.
Mwandishi: Bruce Amani/Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga