1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dola Milioni 100 kuwasaidia wakimbizi wa Afghanistan

24 Julai 2021

Rais wa marekani Joe Biden ameidhinisha dola milioni 100 katika kushughulikia dharura ya wakimbizi inayohusiana na hali nchini Afghanistan

Afghanistan | Binnenflüchtlinge in Laghman
Picha: Omid Deedar/DW

Katika taarifa yake, Ikulu ya White House imesema fedha hizo zitatoka kwenye mfuko wa dharura na ule wa kusaidia wakimbizi kwa lengo la kukabiliana na dharura ambayo haikutarajiwa ya wakimbizi, wahanga wa mzozo na baadhi ya watu ambao wako hatarini kutokana na hali ilivyo nchini Afghanistan.

Fedha hizo zitawasaidia wale wanaoomba visa maalumu SIVs, ambapo karibu raia 20,000 wa Afghanistan walikuwa wakifanya kazi ya ukalimani na kazi nyingine kuisadia Marekani wakati wa vita na sasa wanahofia kuadhibiwa na Taliban. Fedha hizo zinaweza kukusanywa kupitia michango ya ufadhili wa mashirika ya kimataifa, mashirika yasiyo ya kiserikali na yale ya Marekani, iliongeza taarifa hiyo.

Kundi la kwanza la raia na familia zao linatarajiwa kuondolewa nchini Afghanistan kabla ya mwisho wa mwezi huu na watapelekwa katika kambi ya kijeshi ya Fort Lee mjini Virginia wakati wakisubiri mchakato wa visa ukamilike. Utawala wa Biden unatathmini maeneo mengine ya Marekani na nje ya nchi ambako raia hao wa Afghanistan na familia zao wanaweza kupewa makazi. Siku ya Alhamis, bunge la wawakilishi la Marekani lilipitisha sheria itakayoongeza idadi ya watu wanaoweza kupatiwa visa maalumu SIVs na kuwapokea karibu watu 8,000.

Rais Ashraf Ghani na rais Joe Biden walipokutana JuniPicha: Susan Walsh/AP

Kundi la Taliban limeyadhibiti maeneo mengi ya nchi katika miezi ya hivi karibuni, likitumia mwanya wa kuondoka majeshi ya kigeni kufikia mwishoni mwa mwezi Agosti na kuzusha hofu ya mzozo wa kibinadamu. Umoja wa Mataifa hivi karibuni ulikadiria kuwa nusu ya raia milioni 39 wa Afhganistan wanahitaji msaada na kuiomba jumuiya ya kimataifa kuendelea na ufadhili wa kifedha kwa ajili ya nchi hiyo.

Wakati kundi la mwisho la wanajeshi wa Marekani likiendelea kuondoka Afghanistan, Rais Joe Biden amemhakikishia Rais Ashraf Ghani msaada wa kidiplomasia na kibinadamu wakati Taliban ikizidisha shinikizo dhidi ya serikali mjini Kabul.

Agosti 31 ndio utakuwa muda wa mwisho wa vikosi vya Marekani kuondoka Afghanistan baada ya kuingilia mzozo huo ulioanza baada ya mashambulizi ya Septemba 11 mwaka 2001.