Dominique Strauss-Kahn kuwa mgombea kuliongoza Shirika la fedha la kimataifa.
10 Julai 2007Mawaziri wa fedha wa umoja wa ulaya wanaokutana mjini Brussels walikua wakipima ni nani anayefaa kujaza nafasi inayoachwa na Rodrigo Rato wa Uhispania kama mkurugenzi mtendaji wa shiriaka hilo la fedha la kimataifa. Bw Rato alitangaza kwa mshangao wa wengi mwishoni mwa mwezi uliopita kwamba atajiuzulu mwezi Oktoba , akisema anahitaji muda zaidi wa kuwa na familia yake.
Kutokana na makubaliano ya muda mrefu sasa na ambayo yamekosolewa vikali, baina ya Marekani na Ulaya- Marekani humchagua Rais wa benki ya dunia na ulaya yule atakayeliongoza shirika la fedha la kimatafa.
Hata hivyo Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy amekua akimpigia debe Msoshalisti Dominique Strauss Kahn . Strauss –Kahn alikua akitajwa huenda angekua Waziri mkuu pindi mgombea Urais kwa chama cha Kisoshalisti Bibi Segolene Royal amgemshinda Sarkozy katika uchaguzi wa Rais mwezi Mei.
Hoja za waliompinga ni kwamba, tayari wafaransa watatu wamewahi kuliongoza shirika la fedha la kimataifa kwa zaidi ya miaka 30 akatika historia yake ya miaka 61 na pia wafaransa wanaziongoza taasisi tatu tafauti wakati huu, akiwemo Pascal Lamy katika Shirika la biashara duniani WTO, na Jean Claude Trichet kama mkuu wa Benki kuu ya Ulaya . Nyengine ni Benki ya ujenzi na maendeleo ya Ulaya.
Kutokana na kuidhinishwa huko leo na takriban wanachama wote wa Umoja wa Ulaya, baada ya kujiondoa mgombea wa Poland waziri mkuu wa zamani wa nchi hiyo Profesa Merek Belka, Bw Kahn sasa anaweza kuanza kampeni na mashauriano na wanachama wote wa Shirika la fedha la kimataifa .
Awali Uingereza ilishikilia kwamba mkuu mpya atoke nje ya Ulaya, lakini baada ya wengi kumuunga mkono Strauss Kahn, Waziri wa fedha wa Uingereza Sir Alistair Darling alisema”Dominique Strauss-Kahn atakua mgombea mwenye sifa zinazofaa, lakini akasisitiza serikali ya Uingereza inataka kuona ni wagombea gani watatokeza kutoka maeneo mengine, miongoni mwa wanachama wa IMF.
Wadadisi wanasema licha ya kile kinachoonekana ni ushindi kwa rais Sarkozy, hata hivyo kiongozi huyo alikabiliana na hali ngumu jana usiku mbele ya mawaziri wa fedha wa nchi zinazotumia sarafu ya euro, alipotaka kuwashinikiza kuhusu mipango ya nchi yake kukiuka kiwango cha nakisi kilichowekwa kwamba kisizidi 3 asili mia.
Mataifa yote 13 yakanda ya matumizi ya euro yaliafikiana ju ya jukumu la nakisi katika uchumi wao ifikapo 2010, lakini Bw Sarkozy alionya huenda Ufaransa ikahitaji wakati hadi 2012 ili kuurekebisha uchumi wake.. Lakini baada ya vuta nikuvute, kiongozi huyo akaahidi kwamba atajitahidi kufikia lengo lililowekwa la 2010.