Donald Trump aapishwa rais wa 45 Marekani
21 Januari 2017Donald John Trump aliingia madarakani akiwa rais wa 45 wa Marekani jana Ijumaa na kuahidi kufikisha mwisho kile alichosema kuwa ni umwagaji damu nchini Marekani wa viwanda vinavyoota kutu na uhalifu katika hotuba yake ya kuapishwa ambayo ni tamko la siasa kali za mrengo wa kulia na za kizalendo zaidi.
Akionesha ishara ya ukaidi , Trump amesema wafanyakazi wa Marekani wameathirika mno na upelekaji nafasi za kazi nje ya nchi.
"Kuanzia siku ya leo na kuendelea itakuwa Marekani kwanza," rais huyo kutoka chama cha Republican aliwaambia maelfu ya watu waliokusanyika katika uwanja wa taifa kumshuhudia akichukua madaraka kutoka kwa Barack Obama wa chama cha Democratic.
Pamoja na Obama na marais wengine wa zamani watatu wakiwa wameketi karibu, Trump aliushutumu uongozi wa zamani wa Marekani wa kuwatajirisha maafisa mjini Washington kwa mgongo wa familia zenye matatizo nchini Marekani.
Ukionekana mgawanyiko mkubwa nchini humo, maandamano dhidi ya Trump yalifikia hali ya purukushani kubwa mjini Washington. Wanaharakati waliovalia mavazi meusi walivunja madirisha ya vioo ya maduka , walizuwia magari kupita na kupambana na polisi wa kuzuwia ghasia ambao walijibu kwa kurusha mabomu ya kutoa machozi na mabomu ya kushitua. Polisi walisema zaidi ya cwatu 200 walikamatwa.
Watu wachache
Picha zilizochukuliwa kutoka angani za kundi la watu wanaomuunga mkono Trump katika uwanja wa taifa zinaonesha kuwa ni watu wachache waliohudhuria hafla hiyo mchana Ijumaa kuliko ilivyokuwa wakati alipoapishwa rais Barack Obama mwaka 2009.
Makadirio ya watu waliohudhuria hayakupatikana mara moja kutoka kwa polisi.
Hotuba ya baada ya kuapishwa ilikuwa inaakisi hisia halisi za Trump , ikiwa mambo mengi aliyabeba kutoka katika mikutano yake ya kampeni aliyofanya mwaka jana akiwa njiani kuelekea ushindi Novemba 8 dhidi ya mgombea wa chama cha Democratic Hillary Clinton, ambaye alihudhuria sherehe hizo za kuapishwa akiwa na mume wake, rais wa zamani Bill Clinton.
Trump alisema Marekani imevitajirisha viwanda vya mataifa ya kigeni badala ya makampuni ya Marekani, kugharamia majeshi ya nchi nyingine wakati jeshi la Marekani likiporomoka, na kutumia mabilioni ya fedha nchi za nje wakati miundo mbinu ya nchi hiyo ikiharibika.
Wasi wasi wa mataifa ya kigeni
Wakati Trump akijinasibu kama bingwa wa Wamarekani wafanyakazi, kituo cha sera za kodi ambacho ni kituo kinachotoa ushauri bila kujali chama kinakadiria kwamba maendekezo yake ya kodi hayataongeza deni la kiasi cha dola trilioni 7.2 la serikali ya Marekani katika kipindi cha miaka 10 ya mwanzo , lakini mapendekezo hayo yanatarajiwa kuwasaidia tu Wamarekani matajiri.
Kuchaguliwa kwake kulipokelewa kwa wasi wasi na wengi duniani kote, kwa sehemu kutokana na sera za kujitenga za mambo ya kigeni. Katika mahojiano baada ya Trump kuapishwa makamu kansela wa Ujerumani Sigmar Gabriel alisema, "kile tulichokisikia leo ni matamshi mazito ya siasa za kizalendo."
Rais wa Mexico Enrique Pena Nieto alimpongeza Trump kwa kuampishwa, lakini alitahadharisha kwamba utaifa, maslahi ya kitaifa na ulinzi wa Mexico ni masuala ya juu kabisa.
Kiongozi wa kanisa katoliki Papa Francis alimtaka Trump kuongozwa na mfumo wa maadili, akisema ni lazima kuwaangalia masikini na waliotengwa.