1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Donald Trump kujisalimisha rasmi leo

4 Aprili 2023

Ni siku ya kihistoria nchini Marekani, ikiwa ni mara ya kwanza kumuona rais wa zamani Donald Trump akijisalimisha na kufika mahakamani kufuatia mashitaka ya jinai yanayomkabili.

USA I Donald Trump - NCAA Wrestling Championships
Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump alipowasili katika mashindano ya mieleka Machi 18, 2023, huko Tulsa, Okla.Picha: Sue Ogrocki/AP/picture alliance

Donald Trump anakabiliwa na mashtaka ya jinai ya kumlipa fedha taslimu nyota wa filamu Stormy Daniels ili kuficha mahusiano yao ya kimapenzi kabla ya uchaguzi wa mwaka 2016. 

Ni tukio linalowavutia wengi ambao wameonekana kukusanyika katika mitaa na karibu na kuliko mahakama ya Manhattan, New York ili kushuhudia kile ambacho hakijawahi kushuhudiwa nchini humo. Kulingana na waandishi wa habari wa shirika la habari la AP, wapo waliolipia hata viti na nafasi za kusimama ili kujionea kwa macho tukio hili la kihistoria. Wafuasi wake pia hawakuwa nyuma kukusanyika karibu na mahakamani.

Kando ya barabara karibu na mahakama, kulijengwa mahema na wanahabari wakikita kambi kwenye eneo hilo, wapiga picha, wanaume kwa wanawake na bila shaka, mamia ya maafisa wa kulinda usalama. Baadhi ya barabara zinazoizunguka mahakama na mitaa iliyo karibu na mahali ambapo Donald Trump atawasili hii leo zimefungwa. waandishi wa habari wanasema ulinzi ulikuwa umeimarishwa mno katika hali ambayo haijashuhudiwa katika siku za karibuni na hasa wakati baraza kuu la mahakama lilipoingia na hati ya mashitaka.

Soma Zaidi:Trump aelekea New York kabla ya kuanza kwa kesi yake 

Stormy Daniels, mcheza filamu anayedai kulipwa fedha na Trump ili kuficha ukweli kuhusu mahusiano yao. Picha: SMG/ZUMA Wire/picture alliance

Uchunguzi dhidi yake unahusisha malipo ya kiasi cha dola 130,000 alichompa Stormy Daniels ambaye jina lake halisi ni Stephanie Clifford, mzaliwa wa Baton Rouge, Louisiana kupitia kwa wakili wake wa zamani Michael Cohen.

Kulingana na wachambuzi, mwanachama huyo wa Republican anayedai kuwa mhanga anayedhulumiwa kisiasa anatarajiwa kuitumia fursa hii ya kufikishwa mahakamani kujiimarisha na kutafuta uungaji mkono zaidi kwa kuchangisha mamilioni ya dola kwa ajili ya harakati zake za kurejea Ikulu mwakani, licha ya kwamba bado anakabiliwa na msururu wa uchunguzi wa madai mengine dhidi yake.

Soma Zaidi: Trump aapa kupambana mahakamani

Ndani ya mahakama ya Manhattan, waendesha mashtaka wakiongozwa na New York wakili wa wilaya, mDemocrat, Alvin Bragg, wanatarajiwa kuifungua rasmi hati ya mashtaka iliyotolewa wiki iliyopita na baraza kuu la mahakama. Na hapo sasa, ndipo Trump na mawakili wake wa utetezi watakayatambua hasa mashitaka dhidi yake. Hati ya mashtaka ina madai mengi kuanzia ya kughushi biashara na angalau kosa moja la jinai, hii ikiwa ni kulingana na vyanzo viwili vyenye ufahamu na suala hilo, vilipozungumza na shirika la AP wiki iliyopita.

Trump kuyakana madai dhidi yake.

Trump anatarajiwa kuachiliwa huru na mamlaka baada ya kufikishwa mahakamani, kwa kuwa mashtaka dhidi yake hayahitaji dhamana.

Mwanasheria wa wilaya huko Manhattan Alvin Bragg ambaye amekabiliwa na mashambulizi kutoka kwa Trump.Picha: Julia Nikhinson/AP/picture alliance

Aliwahi kushtakiwa mara mbili na Bunge la Marekani ingawa hakuwahi kupatikana na hatia katika Baraza la Seneti. Anakuwa rais wa kwanza wa zamani wa taifa hilo kushitakiwa kwa makosa ya jinai. Amiri jeshi mkuu huyo wa 45  Marekani alisindikizwa na maafisa wa usalama wa taifa kutokea jengo lake la Trump Tower jijini New York. Mwanasheria wa wilaya na mteule wa kwanza mweusi katika mahakama ya Manhattan, Alvin Bragg aliyechukua wadhifa huo tangu Januari 2022 ndiye anayeandika historia hii baada ya yeye na wenzake kufanikiwa kulishawishi baraza kuu la mahakama kumfungulia mashitaka ya kwanza ya uhalifu rais huyo wa zamani.

Trump, nyota wa zamani wa vipindi vya maisha vya televisheni, anatarajiwa kurejea katika makazi yake yaliyopo Mar-a-Lago, Palm Beach, Florida jioni ya leo na kufanya mkutano wa hadhara, ambapo karibu wafuasi wake 500 maarufu wamealikwa. Baadhi ya wabunge wa chama cha Republican wanaomuunga mkono pia wanatarajiwa kuhudhuria.

Trump wakati wote ameuita uchunguzi uliosababisha mashitaka dhidi yake kuwa ulichochewa kisiasa huku akimshambulia wakili Bragg, ambaye anatokea chama cha Democrat. Hata hivyo, mashtaka haya bado hayamzuii Trump kuwania tena urais katika uchaguzi ujao wa mwaka 2024, ingawa wachambuzi wa mambo wanasema inatia doa ofisi nyeti ya rais na hata yeye mwenyewe anayewania tena kurejea madarakani.

Soma Zaidi: Trump kushtakiwa kufuatia malipo kwa Stormy Daniels

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW