1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Donald Trump na msururu wake wa mashtaka mahakamani

22 Machi 2024

Aliyekuwa Rais wa Marekani Donald Trump anakabiliwa na msururu wa mashtaka kwenye mahakama mbambali za nchini humo. Pamoja na mashtaka hayo ni ulaghai na kushawishi matokeo ya uchaguzi.

Uchaguzi wa Marekani 2024  Donald Trump
Donald Trump wa chama cha RepublicanPicha: Meg Kinnard/AP Photo/picture alliance

Kwa jumla Trump, aliyekuwa rais wa 45 katika historia ya Marekani, anakabiliwa na mashtaka 91. Tayari ameshashindwa katika kesi tatu ikiwa pamoja na kutakiwa alipe fidia ya mamilioni ya dola. Licha ya hayo Trump amepania kurudi tena kwenye wadhifa wa urais. Mawakili wake wanajaribu kutumia mbinu za kuchelewesha kesi. Je, atarejea madarakani na hivyo kupewa kinga dhidi ya mashtaka?.

Soma Pia:Trump ataka mdahalo wa uchaguzi na Biden

Mashtaka mazito kabisa dhidi ya Trump yako kwenye mahakama ya mjini Washington DC. Trump anatuhumiwa na mwendesha mashtaka maalum Jack Smith, kutenda makosa manne yanayozingatiwa kuwa uhalifu na idara kuu za sheria za nchini Marekani. Tarehe 6 mwezi Januari mwaka 2021 mashabiki wa Trump walilivamia Bunge ili kuzuia mchakato wa kukabidhi madaraka kutoka kwa Trump kwenda kwa Joe Biden.

Kushoto: Rais wa Marekani Joe Biden. Kulia: Rais wa zamani wa Marekani Donald TrumpPicha: imago images

Mashtaka yanayomkabili Trump

Rais huyo wa zamani wa Marekani anapaswa kujibu mashtaka juu ya kupanga njama, kushawishi matokeo ya uchaguzi na kuchochea uasi. Ikiwa atapatikana na hatia Trump mwenye umri wa miaka 77 atatumikia kifungo jela kwa muda mrefu. Kesi yake ilipaswa kuanza miezi miwili iliyopita lakini kwa sasa shauri lake lipo mbele ya mahakama ya juu.

Mahakama hiyo inapaswa kubainisha ni kwa kiwango gani Trump anaweza kushtakiwa kwa kuzingatia kinga ya kisheria aliyokuwanayo wakati alipokuwa madarakani. Iwapo mahakama hiyo itatoa uamuzi, haijulikani.

Mahakimu walioteuliwa na Trump

Alipokuwa rais, Donald Trump, aliwateua mahakimu watatu kati ya tisa wanaohudumu maisha yao yote. Na kwa kufanya hivyo amejihakikishia idadi kubwa ya mahakimu wahafidhina kwa muda wa miaka mingi ijayo kwenye mahakama hiyo. Na hata ikiwa mahakama itaruhusu kesi dhidi ya Trump isikilizwe haitafanyika karibu na uchaguzi kwa sababu hilo linaweza kuzingatiwa kuwa ni kushawishi matokeo ya uchaguzi.

Sambamba na kesi ya Washington DC,Trump anapaswa pia kujibu mashtaka juu ya kushawishi matokeo ya uchaguzi kwenye jimbo la Georgia.

Katika uchaguzi wa rais wa mwaka 2020 ambapo wagombea walisimama takriban bega kwa bega, Trump alipungukiwa kura 12,000 ili kushinda uchaguzi huo. Ilidhihirika baadae kwamba Trump alimpigia simu msimamizi wa uchaguzi katika jimbo hilo na kumshinikiza achakachue kura. Pia katika hilo rais huyo wa zamani yumo kwenye hatari ya kuhukumiwa kifungo cha muda mrefu jela.

Kesi dhidi ya Trump kuanza lini?

Mwendesha mashtaka wa serikali Fani Willis, amependekeza kesi hiyo ianze mnamo mwezi Agosti. Hata hivyo haijulikani kama itakuwa hivyo. Donald Trump pia anakabiliwa na tuhuma za kumiliki hati nyeti. Mnamo mwaka 2022 polisi wa Florida walizikuta hati hizo kwenye makao yake ramsi, Mar-a-Lago zilizohusu silaha za nyuklia na mipango ya kijeshi ya dharura.

Soma Pia: Mahakama ya Juu ya Marekani yamsafishia njia Trump

Kwa mujibu sheria za Marekani ni marufuku kuzimiliki hati za aina hiyo na kuziweka kwenye nyumba ya mtu binafsi. Trump alikataa kuyarejesha majalada hayo ya siri, licha ya kutakiwa mara kwa mara ayarudishe.

Trump pia anatuhumiwa kuzuia sheria kuchukua mkondo wake. Neno la mwisho bado halijatamkwa, lakini kikosi cha wanasheria wa Trump kimetangaza dhamira ya kukata rufani.