1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Trump kwenye "jaribio jingine la kuuawa"

16 Septemba 2024

Mgombea wa urais nchini Marekani kupitia chama cha Republican Donald Trump yuko salama baada ya risasi kadhaa kufyatuliwa karibu na uwanja wake wa mpira gofu uliopo West Palm Beach, Florida siku ya Jumapili.

Las Vegas | Donald Trump
Mgombea wa Urais nchini Marekani Donald Trump akiwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Harry Reid, baada ya kumaliza kampeni zake mjini Las Vegas, Septemba 14, 2024Picha: Alex Brandon/AP Photo/picture alliance

Shirika la Ujasusi nchini humo, FBI, limesema Trump, alilengwa katika kile walichotaja "jaribio la kumuua." Idara ya Usalama wa Taifa na FBI wamesema wanachunguza tukio hilo lililotokea muda mfupi kabla ya saa nane za mchana, kwa majira ya eneo hilo. 

Risasi zilifyatuliwa kutoka nje ya uzio wa uwanja huo, vimesema vyanzo viwili. Kulingana na maafisa, uwanja huo ulifungwa ili kutoa fursa kwa Trump kucheza.

Baada ya muda maafisa hao wa usalama wa Idara ya Ulinzi wa Viongozi walimuona mtu akiwa na silaha aliyekuwa akichungulia kutokea nje ya uwanja huo kupitia matundu yaliyokuwa kwenye uzio wa uwanja na ambayo yanamwezesha kuona hadi ndani ya uwanja.

Gazeti la Washington Post la nchini Marekani, liliripoti kwamba Trump alikuwa akicheza gofu kwenye uwanja huo wakati kulipotokea tukio hilo na maafisa wa Idara ya Ulinzi wa Viongozi walimkimbiza kwenye chumba maalumu cha mafichoni kilichopo kwenye uwanja huo, hii ikiwa ni kulingana na vyanzo viliwi vilivyozungumzia kile kilichotokea.

Maafisa wa Usalama wakiwa wanahakikisha hali ya ulinzi inaimarika baada ya kuripotiwa kwa kisa hicho cha riisasi karibu na uwanja wa gofu alikokuwa akicheza mgombea wa urais Donald Trump, Septemba 15, 2024Picha: Marco Bello/REUTERS

Soma pia:FBI yachunguza jaribio la mauaji dhidi ya Trump

Ikulu ya White House imesema kwenye taarifa yake kwamba Rais Joe Biden na Makamu wake, Harris wametaarifiwa juu ya tukio hilo na walipata ahueni baada ya kujua kwamba yauko salama.

Harris ameandika kwenye mtandao wa X kwamba "uhalifu hauna nafasi yoyote nchini Marekani."

Mshirika wa karibu kabisa wa Trump, Lindsey Graham amesema amezungumza na Trump baada ya kisa hicho na amemwambia kwamba yuko salama na bado ni miongoni mwa watu wenye nguvu kabisa.

Mtoto wa Trump, Donald Trump Jr, amenukuu jeshi la polisi kwenye eno hilo na kusema kupitia mtandao wa X kwamba, wamekuta bunduki aina ya AK-47, kwenye pori, kamera na begi la mgongoni na linaendelea kuvifanyia uchunguzi.

Taarifa zimesema, Trump alirejea nyumbani kwake Mar-a-Lago.

Donald Trump aliposhambuliwa katika jaribio la kumuu kwenye mkutano wa hadhara huko Pennysylvania, Julai 13, 2024 Picha: Evan Vucci/AP Photos/picture alliance

Ikumbukwe, Trump alijeruhiwa kwa risasi sikioni, katika jaribio la kumuua la Julai 13 huko Pennysylvania na kuibua maswali kuhusiana na usalama wa wagombea urais, miezi kidhaa kabla ya kufanyika uchaguzi unaotarajiwa kuwa na mvutano mkali mnamo Novemba 5, ambapo atakabililiana na Makamu wa Rais wa chama cha Democratic, Kamala Harris.

Kwenye tukio hilo, mtu mmoja aliyehudhuria mkutano wa hadhara ambako shambulizi lilitokea, aliuliwa kwa risasi. Mshambuliaji, kijana wa miaka 20 Thomas Croocks, pia aliuliwa kwa risasi na Usalama wa Taifa.

Kaimu Mkurugenzi wa idara hiyo alisema mwezi Agosti kwamba alifedheheshwa na kitendo hicho kilichoonyesha udhaifu wa idara hiyo, uliotengeneza ombwe la jaribio hilo la mauaji.

Soma pia:Trump kufanya mkutano wake wa kwanza wa nje tangu jaribio la kumuua

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi