Doreen Nabwire: Nyota ndani na nje ya uwanja
31 Januari 2014Bruce Amani alimtembelea Doreen Nabwire katika uwanja wa Geißbockheim, viungani mwa mji wa Cologne, ambako alikutuna naye wakati akifanya mazoezi na wenzake, na kutokana na hadithi yake, Doreen siyo tu nyota ndani na nje ya uwanja wa michezo, bali ni kielelezo kwa wasichana wengi nchini Kenya.
Ni mwendo wa saa moja jioni, katika uwanja wa Geißbockheim, viungani mwa mji wa Köln Ujerumani, ambako ndio makao ya timu za vijana na za wanawake za FC Köln. Doreen Nabwire Omondi pamoja na wachezaji wenzake wanamalizia mazoezi yao ya leo kabla ya mchuano wa kirafiki mwishoni mwa wiki na timu ya Duisburg.
Baada ya kocha wake kupuliza kipyenga cha kukamilisha mazoezi, nilipata fursa ya kukutana na mshambuliaji huyo ambaye ndiye mchezaji pekee mweusi kutoka barani Afrika anayechezea klabu hiyo ya ligi ya daraja ya pili ya Bundesliga. Doreen Nabwire Omondi, mwenye umri wa miaka 26 anasema safari yake kwa hakika imekuwa na panda shuka nyingi tangu alipoanza kuichezea klabu ya Mathare Youths nchini Kenya.
Doreen ambaye ni mama wa mtoto mmoja, alizaliwa katika mtaa wa mabanda wa Korogocho, eneo la Mathare jijini Nairobi, ambako ukimtajia yeyote neno mtaa wa mabanda, kitu kinachomjia akilini kwanza ni masuala kama vile ukosefu wa usalama, kiwango kikubwa cha uhalifu, vijana kujihusisha na dawa za kulevya, miongoni mwa mengine mengi. Hivi vyote Doreen anasema havikuweza kumfanya kushindwa kuendelea kuota ndoto yake ya kuimarisha taaluma yake ya kuwa mwanasoka shupavu.
kando na kuwa nyota ndani ya uwanja, pia ni kielelezo nje ya uwanja. Changamoto zinazowakabili wasichana katika jamii, na hasa wanaoishi katika mitaa ya mabanda, zilimwezesha kuanzisha kikundi kinachofahamika kama GirlsUnlimited, ambacho kinawahamasisha vijana kuhusu namna ya kukuza vipaji vyao na kupitia michezo.
Doreen anahoji kwamba bado hawahi kupata jibu la ni kwa nini soka la wanawake halina umaarufu namna ilivyo michezo mingine ambayo inawapa wanaume na wanawake nafasi sawa za kutamba viwanjani na kuuonesha mashabiki na ulimwengu mzima vipaji walivyo navyo.
Wakati akiwa nchini Uholanzi, kando na kuwa alikuwa anaichezea klabu ya Zwolle, pia alipewa mafunzo ya kuwa mkufunzi wa soka, na akahitimu na shahada ya Diploma. Na sasa anasema kitu ambacho anataka kukifanya wakati atakapozitundika njumu, ni kurudi nchini Kenya, na kuanzisha shule ya kutoa mafunzo ya soka la wanawake, ili kuwapa nao wasichana wengine fursa ya kujiimarisha kama wachezaji nyota, ambao watakuwa maarufu hata kumliko.
Kando na kuwa mchezaji wa FC Köln, yeye pia hufanya kazi na Shirika moja la kijamii mjini Köln linalofahamika kama RheineFlanke, katika kitengo cha kuwahamasisha vijana kuhusu michezo na mabadiliko ya kijamii na maendeleo, kupitia warsha mbalimbali.
Mwandishi: Bruce Amani
Mhariri: Yusuf Saumu