Dortmund bado haijui la kufanya katika Bundesliga
27 Oktoba 2014Viongozi wa Bundesliga Bayern Munich wameshuhudia ushindi wao mara nne mfululizo ulifikia mwisho jana Jumapili baada ya kutoka sare ya bila kufungana na Borussia Moenchengladbach , timu ambayo iko katika nafasi ya pili ya msimamo wa ligi. Bayern Munich ina pointi nne zaidi ya Gladbach wakati VFL Wolfsburg iko katika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 17 sawa na Gladbach, baada ya Wolfsburg kuibamiza Mainz 05 kwa mabao 3-0 jana Jumapili.
Bayern hata hivyo ilibidi kutumia ujuzi wa ziada kuepuka kipigo dhidi ya Gladbach, kama anavyoeleza mlinda mlango wa Bayern Manuel Neuer.
"Nafikiri hatukuonesha mchezo mbovu leo. Gladbach ni timu nzuri. Wamecheza vizuri hadi sasa na wanastahili kuwa katika nafasi ya pili. Ndio maana si aibu kupata sare katika mchezo wa leo."
Kocha mpya wa Schalke 04 Roberto Di Matteo ameshuhudia kikosi chake kikipoteza mchezo wa kwanza tangu aingie madarakani mwezi huu , kwa kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Bayer Leverkusen kwa goli safi kabisa la mchezaji wa kati wa Leverkusen Hakan Calhanoglu.
Borussia Dortmund yazidi kuporomoka
Makamu bingwa msimu uliopita Borussia Dortmund imepoteza tena mchezo wiki hii katika Bundesliga dhidi ya Hannover 96 kwa mara ya nne mfululizo na kuporomoka hadi nafasi ya 15 ikiwa na pointi saba tu kibindoni licha ya rekodi safi kabisa katika Champions League ikiwa imepata ushindi mara tatu bila hata kufungwa bao katika michezo mitatu.
Hali imezidi kuwa mbaya katika Bundesliga, kama anavyosema mlinzi na nahodha wa Borussia Dortmund Mats Hummels.
"Tumepata nafasi nyingi sana, za kupata bao. lakini kwa mara nyingine tena hatukufaulu. Wapinzani wetu wamepata tena bao baada ya kupiga kupiga langoni kwetu mpira wa kwanza. Hiki kwa sasa ni kipindi kigumu mno, ambapo katika bundesliga kila kitu kinakwenda hovyo. Hatujacheza vibaya katika kila mchezo na tumeshindwa mmoja baada ya mwingine. Hii ni vigumu sana kuelezeka."
Wakati huo huo kocha wa Hamburg SV Joe Zinnbauer amerefusha mkataba wake na timu hiyo hadi 2016, baada ya kuiondoa timu hiyo kutoka mkiani mwa ligi.
DFB Pokal
Hata hivyo makamu bingwa Borussia Dortmund inarejea tena uwanjani kesho(28.10.2014) Jumanne katika mchezo wa kombe la ligi DFB Pokal , ambapo ina kibarua kigumu dhidi ya timu ya daraja la pili ya St. Pauli.
Baada ya mchezo huo hapo kesho , Borussia ambayo inasua sua msimu huu inasafiri kwenda Allianz Arena mjini Munich kupambana na mabingwa watetezi na viongozi wa ligi hiyo Bayern Munich katika mchezo wa ligi hapo Jumamosi. Michezo mingine hapo kesho ni kati ya Chemnitz ikipambana na Werder Bremen, Bielefeld ina umana na Hertha Berlin , Aalen inaikaribisha Hannover 96 na Köln iko nyumbani kwa Duisburg.
Siku ya Jumatano(29.10.2014) Bayern inaumana na Hamburg SV , Bayer Leverkusen itaoneshana kazi na Magdenburg na Frankfurt itapimana nguvu na Gladbach.
Mwandishi : Sekione Kitojo / rtre / ZR / afpe
Mhariri: Yusuf , Saumu