1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dortmund, Bayern na Leipzig wote washinda

1 Machi 2021

Borussia Dortmund walipata ushindi wa 2-0 walipocheza na timu iliyopandishwa daraja msimu huu Arminia Bielefeld, magoli yaliofungwa mnamo kipindi cha pili na Mahmoud Dahoud na Jadon Sancho.

Bildkombo | FC Bayern München und Borussia Dortmund

Baada ya kuwa miongoni mwa waliofunga, Sancho alikuwa na haya ya kusema baada ya mechi hiyo.

"Tulikuwa na nafasi kadhaa ila hatukuzitumia kwa hiyo mazungumzo ya muda wa mapumziko yalikuwa kuhusu kuzitumia nafasi hizi. Na tulirudi tukiwa hatari. Ilikuwa muhimu sana kupata bao la kwanza na tukaendelea na hatukusita," alisema Sancho.

Kama mshambuliaji unataka kufunga magoli ila ni sharti uwe na subra

Bayern Munich walipata ushindi wao wa pili katika mashindano yote baada ya kuwalaza FC Köln 5-1 nyumbani kwao Allianz Arena. Robert Lewandowski alitikisa wavu mara mbili katika mechi hiyo na kukaribia sana kuifikia rekodi ya magoli 40 iliyowekwa na Gerd Müller mwaka 1972. Kufikia sasa raia huyo wa Poland ana jumla ya mabao 34. Mshambuliaji wa Cameroon Eric Maxim Choupo-Moting alifunga goli lake la kwanza la Bundesliga tangu asajiliwa na Bayern.

Wachezaji wa Bayern Munich wakisherehekea bao laoPicha: Andreas Gebert/REUTERS

"Ni wazi kama mshambuliaji unataka kufunga au kutengeneza magoli ila wakati mwengine inachukua muda mrefu, inabidi uwe na subra. Nimecheza mpira kwa muda mrefu na nina uzoefu wangu pia, unastahili kuwa mtulivu. Lakini mwisho wa siku, la muhimu ni ushindi wa timu, nataka nipate ufanisi na timu hii. Nina furaha sana na wachezaji wenzangu hapa, tunafanya mazoezi vizuri, tunacheza vizuri na inapofika wakati wa kutoa mchango wangu, inakuwa bora zaidi na ninafurahia kwamba mambo kwangu yametengemaa katika Bundesliga," alisema Choupo Moting.

Na RB Leipzig wanaendelea kuwawekea shinikizo Bayern Munich katika nafasi ya pili kwani baada ya kuwaona mabingwa hao wapya wa dunia wamepata ushindi dhidi ya FC Köln, hawakulegeza kamba walipokuwa wanapambana na Borussia Mönchengladbach, kwani walijizatiti na kufunga goli mnamo dakika ya mwisho ya mechi na kuibuka washindi wa 3-2.

Ushindi dhidi ya Gladbach ulistahili

Mshambuliaji wa Denmark Yusuf Poulsen aliingia kwenye daftari la wafungaji wa mechi hiyo na ni ushindi alioufurahia sana.

Mshambuliaji wa RB Leipzig Yusuf PoulsenPicha: Michael Sohn/AP Photo/picture alliance

"Ni ushindi tuliostahili, tumecheza vizuri sana kwa kuwa tulikuwa chini mabao mawili na hatukujali tukaipindua mechi. Kutokana na mchezo kama wa leo bila shaka tunazidi kujiamini. Gladbach ni timu kubwa na tulistahili kuwafunga na ni wazi kwamba sisi ndio tulikuwa timu bora lakini kwa sasa tunaweka macho yetu kwa kibarua kijacho. Mnamo katikati ya wiki tuna mechi ya robo fainali ya DFB Pokal dhidi Wolfsburg, hii ni mechi kali sana," alisema Poulsen.

Bayern Munich wamewazidi Leipzig na pointi mbili tu katika jedwali la Bundesliga.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW