Dortmund, Leverkusen zapata ushindi
2 Oktoba 2014Borussia Dortmund na Bayer Leverkusen zilifunga magoli matatu kila moja wakati zikipata ushindi katika mechi zao za hatua ya makundi ya Champions League. Dortmund bado haijafungwa goli katika dimba hilo msimu huu.
Vijana hao wa kocha Jürgen Klopp – ambao hawajashinda mechi tatu msimu huu katika Bundesliga – waliandikisha ushindi wa mabao matatu kwa sifuri nyumbani kwa Anderlecht nchini Ubelgiji, huku Adrian Ramos akifunga magoli mawili. Klopp aliamua kumwacha Mkolombia huyo nje ya kikosi cha mwanzo huku Shinji Kagawa akirejea tena na kudhihirisha umuhimu wake kutoka dakika ya mwanzo.
Kagawa alitengeneza goli la kwanza katika dakika ya tatu, kwa kumwandalia krosi Ciro Immobile ambaye alifunga goli lake la pili la Champions League msimu huu.
Leverkusen yatamba
Katika uwanja wa BayArena, Bayer Leverkusen ilikamilisha kile kilikuwa ni jioni nzuri kwa vilabu vya Bundesliga katika Champions League, kwa kuwazaba miamba wa Ureno Benfica magoli matatu kwa moja.
Baada ya kushindwa kutikisa nyavu mwishoni mwa wiki dhidi ya FREBURG, timu hiyo ya kocha Rodger Schmidt ilionekana kuwa hatari katika mashambulizi yake. Stefan Kiessling alifunga goli la kwanza katika dakika ya 18 na kisha dakika tano baadaye, Heung-Min Son akafanya mambo kuwa mbili bila. Eduardo Salvio alifunga goli la Benfica na kuwapa matumaini katika mchezo huo, lakini sekunde chache baada ya hapo mchezaji wa Benfica Jardel alimwangusha Kiessling katika kijisanduku. Hakan Calhanoglu akafunga penalti na kufanya mambo kuwa tatu bila.
Mwandishi: Bruce Amani/DW
Mhariri: Yusuf Saumu