Dortmund yajiimarisha nafasi ya pili
2 Novemba 2015Dortmund iliifunga Werder Bremen magoli matatu kwa moja siku ya Jumamosi. Marco Reus alitikisa wavu mara mbili wakati Henrik Mkhitaryan akifunga moja.
Baada ya Bayern kutekwa sare ya bila bila na Eintracht Frankfurt siku ya Ijumaa, BVB walitumia fursa hiyo kupunguza pengo baina yao. Dortmund sasa wamefunga magoli 18 katika mechi zao nne za mwisho na magoli 64 katika michuano 20 msimu huu chini ya kocha mpya Thomas Tuchel.
Wolfsburg ilisonga hadi nafasi ya tatu baada ya kusajili ushindi wa mbili moja dhidi ya Bayer Leverkusen. Niklas Bendtner na Julian waliifungia Wolfsburg wakati mshambuliaji wa zamani wa Manchester United Javi Hernandez akaifungua Leverkusen. Klaus Allofs ni mkurugenzi wa spoti wa Wolfsburg na anasema "Hizi ni timu mbili ambazo ziko katika kiwango sawa. Tumeliona hilo katika msimu uliopita. Zote zinashindana vikali maana vitu vidogo ndivyo huamua mchezo. Tulijituma sana leo lakini nadhani tulikuwa timu bora katika dakika 90. Ni ushindi muhimu sana leo".
Borussia Moenchengladbach ilipata ushindi wake wa sita mfululizo na kusonga hadi nafasi ya tano baada ya kuibamiza Hertha Berlin 4 moja. Gladbach ilikuwa ikishikilia mkia mwezi wa Septemba baada ya kupoteza mechi tano. Granit Xhaka ni nahodha wa Gladbach na alisema baada ya mchezo "tuna nia na hamu kubwa sana ya kuendelea kufanya bidiii. Tunafanya mazoezi makali kila siku na kuanza kila mchuano kutoka sifuri. Hilo linafanya mwendelezo wetu kuwa mzuri".
Gladbach sasa wako pointi mbili nyuma ya Schalke ambao walitoka sare ya moja moja na Ingolstadt. Huub Stevens alipata pointi moja katika mchuano wake wa kwanza kama kocha wa Hoffenheim baada ya kutoka sare ya bila kufungana na Cologne. Mainz ilitoka sare ya tatu tatu na Augsburg katika mpambano wa kusisimua. Katika matokeo ya jana Stuttgart iliondoka katika nafasi tatu za mwisho katika Bundesliga baada ya kuishinda Darmstadt mbili moja wakati Hanover pia wakiondoka katika eneo hatari la kushushwa ngazi kufuatia ushindi wao wa mbili moja dhidi ya Hamburg.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters
Mhariri: Yusuf Saumu