1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dortmund yaanza kampeni ya ligi ya mabingwa kwa ushindi

19 Septemba 2024

Mshambuliaji wa pembeni Jamie Gittens aliingia kama mchezaji wa akiba na kufunga mabao mawili katika dakika 15 za mwisho na kuisaidia klabu hiyo ya Ujerumani kupata ushindi wa 3-0 dhidi ya Club Brugge ya Ubelgiji.

Bundesliga | SC Freiburg vs. Borussia Dortmund | Jamie Bynoe-Gittens
Mshambuliaji wa pembeni wa Borussia Dortmund Jamie GittensPicha: Revierfoto/IMAGO

Dortmund, iliyopoteza mechi ya fainali ya michuano hiyo ya Ulaya msimu uliopita mbele ya miamba Real Madrid, ilifunga bao la kwanza kunako dakika ya 76 kabla ya Gittens kufunga bao lake la pili katika dakika ya 86 ya mchezo.

Mshambuliaji mpya Serhou Guirassy aliyejiunga na Dortmund akitokea Stuttgart ambapo alifunga mabao 28 katika mechi 28 za ligi kuu ya Bundesliga msimu uliopita, alifanyiwa madhambi kwenye kisanduku cha 18 na kufunga penalti ya dakika za lala salama.

Gittens amekiambia kituo cha habari za michezo cha DAZN kuwa, anajisikia vizuri baada ya kupata ushindi na kwamba aliingia uwanjani akiwa na nia ya kufanya mabadiliko kwenye mchezo.

Soma pia: Champions League yarudi tena, nani atatinga robo fainali?

Nahodha wa Dortmund Emre Can amemwagia sifa raia huyo wa Uingereza mwenye umri wa miaka 20, akieleza kuwa alileta nguvu mpya na kusaidia kubadili mwelekeo wa mchezo.

Nuri Sahin mwenye umri wa miaka 36 na ambaye ni kocha mwenye umri mdogo zaidi katika michuano ya mwaka huu ya ligi ya mabingwa barani Ulaya, alifanya mabadiliko ya wachezaji watatu kutoka kikosi cha mwishoni mwa wiki katika pambano dhidi ya Heidenheim, ikiwa ni pamoja na kumweka benchi Guirassy ambaye anaendelea kurudisha fomu yake baada ya kuwa nje kwa muda mrefu kutokana na jeraha.

Ushindi huo wa 3-0 dhidi ya Club Brugge unaifanya Dortmund kuwa timu ya kwanza katika historia ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya kucheza dhidi ya timu hiyo mara tano bila ya kuruhusu bao.

Manchester City yabanwa pumzi na Inter Milan ugani Etihad

Wachezaji wa Manchester City Kevin De Bruyne na Erling HaalandPicha: MartinxRickett/PA Images/IMAGO

Na katika uwanja wa Etihad nchini England, Manchester City imeanza kampeni yao ya ligi ya mabingwa barani Ulaya kwa mguu mbaya baada ya kulazimishwa sare ya bila kufungana na klabu ya Inter Milan.

Katika marudio ya fainali ya mwaka 2023 ambayo vijana wa Pep Guardiola waliibuka kidedea mjini Istanbul, wakati huu Inter Milan ilionyesha ukakamavu uwanjani na kuziba mianya yote ya safu ya ulinzi licha ya kukabiliwa na shinikizo kubwa hasa katika kipindi cha pili.

Manchester City licha ya kubebwa na mashabiki wa nyumbani, walishindwa kufurukuta mbele ya wapinzani wao wa Italia huku jeraha la kiungo wao Kevin de Bruyne lililomlazimisha kuondolewa uwanjani wakati wa mapumziko ya kipindi cha kwanza likififisha matumaini ya kuondoka na alama tatu.

Soma pia: Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu bila ya Messi na Ronaldo

Mshambuliaji matata Erling Haaland, anayesaka bao lake la 100 akiwa na pamba za Manchester City, alidhibitiwa kwa ustadi na safu ya ulinzi ya Inter Milan.

Kocha wa Inter Milan Simone Inzaghi ameeleza masikitiko kutokana na wachezaji wake kukosa nafasi za wazi za kufunga mabao japo ameridhika na sare hiyo.

Ingawa sare ya 0-0 ugenini ni matokeo mazuri kwa Inter Milan, Inzaghi anahisi timu yake ilikuwa na fursa ya kuibuka na ushindi.

Inter Milan sasa inalekeza nguvu zake katika mechi ya dabi dhidi ya watani wao AC Milan nyumbani San Siro katika mechi ya ligi kuu ya Italia mnamo siku ya Jumapili wakati Manchester City wakiwa na kibarua kigumu dhidi ya washika bunduki Arsenal siku hiyo hiyo japo kuna mashaka juu ya kupatikana kwa Kevin de Bruyne kwenye mtanange huo muhimu wa ligi kuu ya Premia.