1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dortmund yashinda katika hali ya huzuni

14 Machi 2016

Borussia Dortmund jana imepata ushindi wa 2-0 dhidi ya Mainz lakini mchuano huo uligubikwa na kifo cha shabiki mmoja mwenye umri wa miaka 80 kilichotokea uwanjani

Fußball Bundesliga Borussia Dortmund v FSV Mainz 05
Picha: Reuters/I. Fassbender

Shabiki huyo mzee wa Dortmund alizirai kutokana na kile kinachoshukiwa kuwa ni mshutuko wa moyo wakati akishuhudia mchuano huo ndani ya uwanja wa Signal Iduna Park uliokuwa na mashabiki 81,000. Shabiki wa pili pia alizirai, lakini akapewa huduma ya kwanza wakati akiwa njiani kupelekwa hospitali.

Marco Reus alifunga bao katika dakika ya 30, lakini sasa kipindi cha pili kilisalia kimya wakati habari za kifo hicho zikisambazwa kutoka kwa shabiki mmoja hadi mwingine. Shinji Kagawa alifunga la pili katika dakika 73 lakini kulikuwa na ukimya tu. Huyu hapa mshambuliaji wa BVB Marco Reus "Hatukuweza kufahamu chochote uwanjani. Tulikuwa na hofu na kukerwa sana kwa nini kipindi cha pili kilikuwa na ukima tangu mwanzoni. Nilizungumza na refarii mara mbili aliyeniuliza nini mbaya. Nikasema sijui chochote. Baada ya mechi maafisa wetu walituambia kuwa mtu mmoja alizirai wakati wa mechi na hilo ni tukio baya lililougubika mchezo na wala sio matokeo".

Mara baada ya kipenga cha mwisho kupulizwa, timu a Dortmund ilikusanyika wakati mashabiki wakiimba wimbo wa klabu hiyo wa “You'll Never Walk Alone” yaani “Hautokuwa Peke Yako”.

Ushindi huo unaiwacha Dortmund katika nafasi ya pili pointi tano nyuma ya Bayern Munich. Awali, Bayer Leverkusen ilipata ushindi wa bao moja kwa sifuri dhidi ya Hamburg, bao lililofungwa na mchezaji wa Hamburg katika lango lake. Kocha wa Hamburg Bruno Labbadia alisema wanapaswa kujilaumu wenyewe "Hatukuweza kuingia kabia mchezoni, tulichukua muda mwingi kutulia hata ingawa tulijua kilichokuwa tukisubiri. Bila shaka katika kipindi cha pili tuliimarika, tukawa na nafasi nyingi sana. Na kila mara Lakini mlinda mlango hupata motisha kama alivyokuwa leo Bernd Leno na tukabaki na mikono vichwani. Na ndio maana leo tumekata tamaa kabisa"

Mashabiki wakiimba wimbo wa "Hautokuwa Peke Yako"Picha: Reuters/I. Fassbender

Jumamosi, Bayern Munich iliibamiza Werder Bremen 5-0 na kujiimarisha kileleni. Wolfsburg ililambishwa moja bila na Hoffenheim. Hanover inakabiliwa na kitisho cha kushushwa ngazi baada ya kichapo cha mbili sifuri na Cologne. Ron-Robert Zieler ni mlinda mlango wa Hanover "Ninaweza kuelewa wanachohisi mashabiki hadi wakaonyesha wazi hasira yao kwa kuizomea timu ili kufanya jukumu lake. Leo ulikuwa mchezo muhimu ambao tumeupoteza tena. Hili ni janga kubwa kabisa. Sisi kama timu hatujafanya vya kutosha lazima ukweli usemwe wazi".

Kocha mpya wa Eintracht Frankfurt Niko Kovac alipata pigo la tatu bila dhidi ya Borussia Moenchengladbach katika mchuano wake wa kwanza. Augsburg ilitoka sare ya 2-2 na Darmstadt.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/AP/Reuters
Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman