1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Borussia Dortmund yabanwa 1-1 na Augsburg

16 Desemba 2023

Borussia Dortmund imelazimishwa sare ya 1-1 na Augsburg Jumamosi na kufikisha mechi tatu za ligi bila ushindi na kupoteza zaidi katika mbio za kuwania taji la Bundesliga.

Fussball Bundesliga | Augsburg - Borussia Dortmund
Marco Reus (wapili kushoto) akijarivu kufunga wakati wa mechi ya Bundesliga kati ya Augsburg na Borussia Dortmund mjini Augsburg, Desemba 16, 2023.Picha: Michaela Rehle/AFP/Getty Images

Klabu hiyo ya bonde la Ruhr, ikiwa na ushindi mmoja pekee katika mechi saba zilizopita za ligi, iko nafasi ya tano kwa pointi 26, 10 nyuma ya viongozi Bayer Leverkusen ambao wana nafasi ya kuendeleza uongozi wao watakapocheza na Eintracht Frankfurt Jumapili.

Mabingwa Bayern Munich, waliopo nafasi ya pili wakiwa na pointi 32, watawakaribisha VfB Stuttgart wanaoshika nafasi ya 31, Jumapili.

RB Leipzig waliingia katika nafasi ya tatu wakiwa na 32 kwa ushindi wa 3-1 dhidi ya Hoffenheim. Emil Forsberg wa Leipzig alifunga kabla ya Mswidi huyo kuhamia New York Red Bulls kwa mkataba wa miaka miwili Januari 1.

Ligi hiyo itapumzika baada ya mechi za wiki ijayo hadi Januari 12.

Soma pia: Mashabiki: Dortmund ilikosa nafasi ya kuchukuwa msimamo wa wazi kwa usajili wa Nmecha

"Matokeo hayo kwa hakika hayaturidhishi," alisema kocha wa Dortmund Edin Terzic, ambaye amekuwa kwenye shinikizo kubwa.

"Kabla ya mchezo tulisema tunataka na tunahitaji pointi sita kutoka mechi mbili za mwisho zilizosalia mwaka huu."

"Hatukufanikiwa leo ingawa tulikuwa na nafasi za kutosha za kushinda. Kwa 1-1 hali yetu kwenye msimamo haijaimarika. Lakini siwezi kuwalaumu wachezaji. Tulionyesha kuwa tulijaribu kila kitu kushinda," alisema.

Ermedin Demirovic aliwaweka wenyeji Augsburg mbele baada ya kumpiga chenga beki Nico Schlotterbeck na kufunga dakika ya 23.

BVB imecheza mechi tatu bila ushindi.Picha: Bernd Feil/MIS/IMAGO

Augsburg wazidi kujiimarisha

Bao lao la kuongoza lilidumu kwa dakika 12 pekee, baada ya Donyell Malen kuungana vyema na Niclas Fuellkrug na kupiga shuti la chini chini wakati Dortmund wakijaribu kurejea kutokana na kipigo cha Leipzig wiki iliyopita.

Soma pia:Terzic: Tulifanikiwa kuwadhibiti Leverkusen kimbinu 

Augsburg inayoendelea kujiboresha, na ambayo imepoteza mara moja pekee katika mechi zao nane za mwisho za Bundesliga chini ya kocha Jess Thorup, walipata nafasi tatu mfululizo katika mwanzo mzuri wa kipindi cha pili kabla ya Dortmund kujibu shuti kutoka kwa Fuellkrug ambalo lilitoka nje kidogo ya lango.

Dortmund, ambao walipata nafasi nyingi katika kipindi cha pili, walikaribia kwa uchungu kufunga bao la ushindi wakati mchezaji wa kimataifa wa Ujerumani Fuellkrug alipounganisha kwa ustadi krosi ya Thomas Meunier.

Lakini voli yake ya juu katika dakika ya 87 ilipanguliwa wavuni na kipa Finn Dahmen, ambaye pia alimzuwia Malen dakika moja kabla.